Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msigwa: Katiba Mpya ndio mwarobaini kulinda rasilimali za Taifa

Msigwa+px (600 X 303) Msigwa: Katiba Mpya ndio mwarobaini kulinda rasilimali za Taifa

Thu, 3 Aug 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa, Peter Msigwa amewaomba Watanzania wote bila kujali itikadi, dini wala maeneo ya Kijiografia kuunga mkono hoja ya kudai Katiba Mpya ikayounda taasisi imara na kuwapa wananchi mamlaka ya kulinda rasilimali za Taifa.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Lulembera Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Msigwa ambaye ni mbunge wa zamani wa Iringa mjini amesema Katiba ya sasa imetoa mamlaka na madaraka makubwa kwa viongozi akiwemo Rais anayetajwa kuwa ndiye mdhamini wa ardhi yote na anaweza kuitwaa na kuigawa kwa yeyote wakati wowote.

‘Kwa Katiba yetu ya sasa, madaraka makubwa yamemilikishwa kwa kikundi kidogo cha watu ambao wanatumia vibaya madaraka yao…katiba hii haiwezi kulinda rasilimali za Taifa. Tunawaomba Watanzania mtuunge mkono katika harakati za kudai na kuleta mabadiliko ya kimuundo, kimfumo, kisera na kifikra,’’ amesema Msigwa

Amesema Taifa linahitaji Katiba Mpya itakayoweka mipaka na kuwajibisha viongozi wote wanaokiuka viapo vyao ikiwemo kutumia vibaya mali, fedha na rasilimali za Taifa.

‘’Viongozi lazima waishi wakihofia nguvu ya wananchi kupitia Katiba; kwa bahati mbaya, Katiba yetu ya sasa inawafanya viongozi kuwa miungu watu wanaoogopwa na wananchi waliowakasimia madaraka,’’ amesema

Amesema kutokana na umuhimu wa mabadiliko ya kiuongozi na hoja ya Katiba Mpya, Chadema inatekeleza operesheni ‘’+255Katiba Mpya Okoa Bandari Zetu’’ iliyozinduliwa Julai 28, 2023 mjini Bukoba na kufuatiwa na mikutano kadhaa ya hadhara inayofanyika katika mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza.

“Tumekuja hapa Mbogwe na tutaenda kila kona ya nchi kuwaondolea wananchi hofu katika madai ya masuala muhimu yenye maslahi kwa Taifa ikiwemo dai la Katiba Mpya, maisha na uongozi bora,’’ amesema

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche amesema hali duni kimaisha waliyonayo Watanzania ni matokeo ya Katiba iliyopo isiyotoa mamlaka yote kwa umma katika maamuzi ya mambo yanayowahusu ikiwemo matumizi ya rasilimali za Taifa.

‘’Tanzania tumejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwemo utajiri wa aina mbalimbali za madini, mbuga za wanyama, misitu, ardhi yenye rutuba na hali nzuri ya hewa lakini tumeendelea kuwa maskini hata baada ya zaidi ya miaka 60 ya Uhuru. Lazima tuamue mustakabali wetu kwa kuikiondoa madarakani CCM kupitia sanduku la kura,’’ amesema Heche

Mbunge huyo wa zamani wa Tarime Vijijini amedai matatizo ya kiuchumi nchini hayawezi kuondolewa na watu wale wale walioyaleta wenye fikra na sera zile zile; hivyo ni lazima kufanyike mabadiliko kuleta sera na fikra mpya kwa kukipumzisha CCM.

Chanzo: mwanachidigital