Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msekwa azungumzia Spika Ndugai kuwalinda wabunge wa Chadema

30012 Pic+msekwa Msekwa azungumzia Spika Ndugai kuwalinda wabunge wa Chadema

Wed, 13 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SIKU moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwafukuza wabunge wake wanne na Spika wa Bunge kusema atawalinda, Spika mstaafu, Pius Msekwa na baadhi ya wachambuzi, wamezungumzia hali hiyo.

Wabunge waliofukuzwa ni Anthony Komu (Moshi Vijijini), Joseph Selasini (Rombo), David Silinde (Momba) na Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini) ambao wamefukuzwa kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na kauli za kashfa na kejeli dhidi ya chama na uongozi wake na kukiuka makubaliano.

Hata hivyo wakati akihitimisha bunge juzi, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alikaririwa akisema yeye ndiye mwenye dhamana ya kuwaapisha wabunge hivyo, wabunge wa Chadema wanaoingia bungeni wasitishwe na mtu yeyote.

MTANZANIA lilimtafuta Msekwa kujua tafsiri za maamuzi hayo lakini alisisitiza kuwa uamuzi wa spika hauhojiwi.

“Haina tafsiri yoyote, ni spika amesema sasa unataka kutafsiri maneno ya spika, ametoa uamuzi wake sasa unauhoji uamuzi wa spika kwanini, una haki gani ya kuhoji maamuzi ya spika…si sahihi.

“Kwanini msihoji uamuzi wa wale waliofukuzwa, si wamewafukuza kwa madaraka waliyonayo…kwa katiba waliyonayo,” alisema Msekwa.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema Spika anapaswa awe mstari wa mbele kusimamia sheria na katiba za nchi ili kudumisha mshikamano.

“Moja kwa moja wamepoteza ubunge kufuatana na katiba na sheria za Tanzania kwa sababu sheria ya nchi yetu mbunge lazima awe amedhaminiwa na chama cha siasa.

“Utawala wa sheria na katiba ndiyo msingi wa kuleta heshima ya nchi na mshikamano sasa tunashangaa spika anapindisha sheria na katiba za nchi kwa sababu tu ya kisiasa, si jambo zuri anapaswa awe mstari wa mbele kusimamia sheria na katiba za nchi,” alisema Profesa Mpangala.

Akizungumza kwa njia ya mtandao juzi, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema katika kikao chake kilichofanyika Mei 9 na Mei 10 kwa njia ya video, kwa mujibu wa katiba ya chama, sifa za uanachama wa Chadema kwenye kifungu cha 5.15 cha katiba kinasema mwanachama wa Chadema lazima awe anakubaliana na itikadi na falasafa ya chama.

“Kwa hiyo Komu na Selasini kwa nyakati tofauti walijitokeza mbele ya waandishi wa habari na kutangaza kwamba haakubaliani na itikadi ya Chadema na wanakubaliana na itikadi ya chama kingine na baada ya hapo wameendelea kutoa lugha za kejeli dhidi ya chama na uongozi wake. Hivyo Kamati Kuu ya chama katika kikao chake kimefikia uamuzi wa kuwafuta uanachama,” alisema.

Mnyika alisema wabunge David Silinde (Momba) na Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini) siyo tu wamekiuka maagizo ya chama, bali pia wamekuwa wakijitokeza kwenye vyombo vya habari na njia nyingine za mawasilianao na kutoa maneno ya kashfa na kejeli dhidi yamaagizo ya chama na ya viongozi wa chama.

Katibu Mkuu huyo wa Chadema, alisema kuwa azimio la nne la kamati kuu iliamua kuhusu wabunge wengine ambao walikwenda kinyume na maagizo na makubaliano ya chama na wabunge lakini hawajaonesha utovu wa nidhamu wa ama kukikashifu au kukikejeli chama na uongozi wake.

“Hawa kamati kuu ya chama imeazimia kwamba watakiwe kujieleza ni kwa vipi wasichukuliwe hatua zaidi kwa kukiuka hayo maagizo na makubaliano ya chama na wabunge wafuatao wanaingia kwenye kundi hili.

“Hao ni Suzan Masele, Joyce Sokombi, Latifa Chande, Lucy Mlowe, Sware Semesi, Jafari Michael, Peter Lijualikali, Willy Kambalo, Rose Kamili, Sabrina Sungura na Anne Gideria ambao watatakiwa kujieleza kuhusu uamuzi wao wa kukiuka makubaliano kati ya wabunge na uongozi wa chama.

“Hao wamepewa nafasi hiyo ya ziada kwa sababu tu baada ya kukiuka huko maagizo hawajaonekana mbele ya vyombo vya habari wakihujumu chama,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live