Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msekwa: Kuna hitaji, sababu za mfumo wa vyama vingi

98698 Pic+uchaguzi Msekwa: Kuna hitaji, sababu za mfumo wa vyama vingi

Wed, 11 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanzania ilirejea kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 karibia miaka 32 tangu uchaguzi wa mwisho wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1960.

Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, Watanzania wameshuhudia chaguzi sita , tatu zikiwa zenye ushindani mkali kati ya chama tawala, CCM na vyama shindani ambavyo wengi huita vya upinzani.

Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995, Augustino Mrema kupitia NCCR-Mageuzi alitoa ushindani mkali dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa aliyeibuka mshindi na kuongoza Serikali ya awamu ya tatu.

Ushindani mwingine mkali ulishuhudiwa mwaka 2010 kati ya mgombea wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Jakaya Kikwete aliyekuwa akiwania awamu ya pili ya kuongoza Serikali ya Awamu ya Nne.

Mwaka 2015 ndipo kilele cha ushindani uliposhuhudiwa kati ya Edward Lowassa wa Chadema aliyekuwa akiwakilisha vyama vilivyounda Ukawa na Rais wa sasa, John Magufuli wa CCM.

Ushindani huo ulitegemea mazingira ya kisiasa yaliyokuwapo katika kila kipindi, kama anavyoeleza Spika mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa.

Pia Soma

Advertisement
Mwanasiasa huyo mkongwe anasema siasa ya mfumo wa vyama vingi ni hitaji la wakati unaotoa fursa kwa wananchi kuonyesha hisia zao, iwe kupendezwa au kuchukizwa na uongozi ulioko madarakani.

“Tanzania haiwezi na kwa hakika haifai kurejea kwenye mfumo wa chama kimoja cha siasa kwa sababu mfumo wa vyama vingi ni hitaji la jamii kulingana na wakati,” anasema Msekwa.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Nansio, Ukerewe wiki iliyopita, Msekwa anasema uchaguzi katika mfumo wowote hutoa fursa kwa wapiga kura kutoa hisia zao.

“Hata huu uchaguzi wa mwaka 2020, wapiga kura watafanya maamuzi kulingana na utendaji wa Serikali kwa kuonyesha kuridhika au kuchukizwa,” anasema.

Historia ya chaguzi

Msekwa anasema fursa kwa wapiga kura kuonyesha hisia zao kupitia sanduku la kura ni miongoni mwa sababu za msingi za uchaguzi tangu wakati wa mfumo wa vyama vingi ndani ya Tanganyika chini ya Ukoloni, Tanganyika baada ya ukoloni na Tanzania chini ya Tanu na CCM.

Akijaribu kuvuta kumbukumbu, mkongwe huyo wa siasa nchini anasema kuna chaguzi nyingi zimefanyika ndani ya Tanganyika chini ya ukoloni na Tanganyika huru. Miongoni mwazo ni ule ya mwaka 1958 ambao anasema hakuushiriki kwa sababu alikuwa mwanafunzi.

“Mwaka 1959, uchaguzi mwingine wa vyama vingi ulifanyika kwa lengo la kuonyesha mgawanyo na nguvu za vyama vya siasa. Uchaguzi huu ni maarufu kama uchaguzi wa kura tatu kwa maana ya kuchagua mgombea mmoja mwafrika, mhindi na mzungu na wagombea wa Tanu walishinda katika majimbo yote 10,” anasema.

Uchaguzi mwingine wa vyama vingi anaokumbuka katibu mtendaji huyo wa zamani wa CCM ni ule wa mwaka 1960 ambapo wagombea wa Tanu waliibuka na ushindi katika majimbo yote 71, yakiwamo yale yaliyotengwa maalum kwa ajili ya wazungu na wahindi.

Anasema wagombea Wazungu walitengewa majimbo 10, wakati Wahindi walikuwa na majimbo 11 huku majimbo 50 yakiwa ya wazi kwa vyama vyote vya siasa ambapo wagombea 58 wa Tanu walipita bila kupingwa na wengine 13 wakiibuka washindi katika majimbo yaliyokuwa na wagombea wa vyama vingine.

“Kufikia hapo, wakoloni hawakuwa na namna zaidi ya kukabidhi Uhuru kwa Tanganyika,” anasema.

Wakati Tanganyika inajipatia uhuru wake mwaka 1961 kulikuwa na vyama vingi vya siasa vya Tanganyika African National Union (TANU) kilichoanzishwa Julai 1954, United Tanganyika Party (UTP) kilichoanzishwa Februari 1956, All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT) kilichoanzishwa Julai 1959 na African National Congress (ANC) kilichoanzishwa Juni 1958.

Vyama hivi vilishiriki katika chaguzi za Baraza la Kutunga Sheria (Legco) mwaka 1958, 1959 na 1960.

Hata hivyo, ni vyama viwili tu—TANU na ANC—vilishiriki katika Uchaguzi Mkuu wa kumpata Rais wa Tanganyika uliofanyika Novemba 1, 1962.

Baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, ndipo ukaja utaratibu unaoendelea hadi sasa wa madiwani, wabunge na Rais kuchaguliwa kila baada ya miaka mitano.

Msekwa anasema uchaguzi wa kwanza baada ya Uhuru ulifanyika mwaka 1965, chini ya mfumo wa chama kimoja kupitia Katiba ya muda ya mwaka 1964 iliyoandikwa baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Sababu kwenda chama kimoja

Akizungumzia mabadiliko hayo, Msekwa anasema pamoja na sababu zingine, hitaji la kujenga Taifa lenye umoja, undugu, mshikamano na utangamano ilikuwa moja ya busara ya kwenda kwenye mfumo wa chama kimoja.

“Baadaye kukawepo mfumo wa kushindanisha wagombea ndani ya chama kimoja. Kwanza kuondoa uwezekano wa mtu kupita bila kupingwa; na pili ni kutoa fursa na haki kwa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka,” anasema Msekwa.

“Hata hivyo, matokeo ya chaguzi zote kwenye mfumo wa vyama vingi kabla na baada ya Uhuru pia yalidhihirisha kuwa hakukuwa na chama cha siasa kilichokuwa na nguvu na uwezo wa kukabiliana na Tanu,” anasema.

Hitaji la vyama vingi

Pamoja na sababu hizo muhimu, “hitaji la kurejea kwenye mfumo wa vyama vingi lilionekana wakati wa Tume ya Jaji Francis Nyalali ambayo mimi nilikuwa miongoni mwa wajumbe.

“Hii ilikuwa ni kutoa fursa ya kushindanisha hoja na sera ya vyama kushawishi wapiga kura. Hitaji hilo bado liko hai hadi sasa.

“Kwa hivyo, bado naamini Tanzania itaendelea kuwa Taifa la mfumo wa vyama vingi kwa sababu ya wakati, mahitaji ya jamii na mazingira ya siasa za kidunia,”anasema.

Hata hivyo, nguli huyo wa siasa nchini anaonya kuwa fursa hiyo ya kunadi sera na hoja inatakiwa kutumika vizuri bila kufarakanisha Taifa.

“Wanasiasa washindane na kupingana kwa hoja bila kupigana, maana nchi yetu ni moja, yenye watu wamoja wanaoishi kwa umoja, undugu na mshikamano,” anasema.

Wapinzani kususia uchaguzi

Msekwa anazungumzia matukio ya vyama vya upinzani kususia uchaguzi, akisema “ni dynamics (mitazamo) za kisiasa kwa wapinzani kususia uchaguzi, lakini kwa maoni yangu kususia uchaguzi ni kuwanyima wapiga kura haki na fursa ya kumchagua mgombea wanayemtaka,” anasema.

“Kitendo cha wagombea wote wa vyama vya upinzani kujitoa kwenye uchaguzi ni kutoa fursa kwa wagombea wa CCM hata wale wasio chaguo la wananchi kupita bila kupingwa,” anasema.

Anavisihi vyama vya upinzani kuacha tabia ya kujitoa ili kuwapa wananchi fursa ya kikatiba ya kupiga kura kuchagua viongozi wanaowataka.

Anasema miaka ya nyuma utaratibu wa kushindanisha wagombea ndani ya chama kimoja uliwezesha wananchi kuwapima wagombea na kupata kiongozi bora na papo hapo kupata nafasi ya kuonyesha hisia kwa kuwaondoa viongozi ambao hawakujibu matakwa na matarajio yao.

Hata baada ya Katiba mpya ya mwaka 1977 inayotumika hadi sasa baada ya kufanyiwa marekebisho kadhaa, chaguzi za mwaka 1980, 1985 na 1990 pia zilifanyika chini ya mfumo wa chama kimoja.

Ilivyokuwa kwenda chama kimoja

Haikuwa kazi rahisi kwa Tanza kutoka mfumo na vyama vingine kwenda chama kimoja.

Karibu miaka miwili baada ya Uhuru wa Tanganyika, Rais Julius Nyerere alikielekeza chama chake cha TANU kuunda Tume ya kuangalia uwezekano wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya chama kimoja cha siasa.

Tume hiyo iliundwa Januari 28, 1964 kupitia uamuzi wa kikao cha Halmashauri Kuu ya TANU cha Januari 14, 1963 ikiwa na wajumbe 13 waliojumuisha uwakilishi wa makundi yote -- wazungu, waasia na waafrika chini ya uenyekiti wa makamu wa Rais wa wakati huo, Rashidi Kawawa, katibu wake akiwa Amon Nsekela.

Wajumbe wengine walikuwa ni aliyekuwa waziri wa Mambo ya Nje, Oscar Kambona, Waziri wa Sheria, Sheikh Amri Abeid Kaluta, Lucy Lameck, Bhoke Munanka, Dk Leader Stirling (mbunge); Chifu Petro Marealle, Roland Brown (aliyekuwa mwanasheria mkuu wa Serikali); Makamu Wakili Mkuu wa Serikali, Mark Bomani.

Wengine walikuwa ni makamu mwenyekiti wa Bodi ya Kilimo Tanganyika, Hero Raymond Msefya, Joseph Augustine Namata na mjumbe aliyejulikana kwa jina moja la Mustafa.

Baadaye wajumbe wengine Mtoro Rehani, Hamed Amir, Hamisi Masoud na Ahmed Hassan Diria waongezwa.

Ripoti ya Tume iliwasilishwa Machi 22, 1965, ilijadiliwa na wajumbe kutoka TANU ya Tanganyika na Afro-Shirazi Party (ASP) ya Zanzibar na kuidhinishwa.

Baadaye muswada wa sheria uliuliwasilishwa bungeni na kutungwa sheria na Katiba kuruhusu nchi kuwa na mfumo wa chama kimoja cha siasa.

Kesho usikose kusoma

Chanzo: mwananchi.co.tz