Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msambatavangu afunguka kuwekwa kiporo CCM

32859 Pic+msambavatangu wenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu

Sat, 22 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu amesema anakubaliana na uamuzi wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho iliyomweka chini ya uangalizi usiokuwa na ukomo.

Hivi karibuni, NEC chini ya uenyekiti wa Rais John Magufuli iliwasamehe na kuwarejeshea uanachama wenyeviti wanne wa CCM wa zamani huku Msambatavangu akiwekwa chini ya uangalizi hadi pale chama kitakapojiridhisha juu ya mwenendo wake wa maadili.

“Uamuzi nimeupokea vizuri, naishukuru NEC, namshukuru mwenyekiti wa chama kwa sababu hata kufikiria tu kuisoma barua yangu ni hatua nzuri. Nipo tayari kuwa chini ya uangalizi, ninafahamu wana nia njema,” alisema juzi akizungumza kwa simu na mwandishi wetu.

“Pengine wanataka kujiridhisha na vitu fulani au kuna mambo wanayaweka sawa, kwa hiyo naona ni utaratibu wa kawaida.”

Machi 2016, Msambatavangu alivunja kikao cha kamati ya siasa ya Mkoa wa Iringa na kuahirisha kwa muda usiojulikana kile cha halmashauri ya mkoa huo baada ya wajumbe waliohudhuria kushinikiza kuwajadili wanachama wanaodaiwa kukisaliti chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Vuguvugu la Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo liliwaathiri wenyeviti watano wa chama hicho ambao walivuliwa uanachama katika uamuzi wa vikao vya chama hicho.

Hata hivyo, juzi NEC iliamua kuwasamehe wanne baada ya kujiridhisha na maombi ya barua zao za kuomba kusamehewa kutokana na makosa ya kimaadili waliyotenda wakiwa viongozi.

Wenyeviti wa mikoa walisamehewa ni Ramadhani Madabida Mkoa wa Dar es Salaam, Erasto Kwirasa (Shinyanga), Christopher Sanya (Mara) na Salum Madenge ambaye alikuwa mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni.

Akitoa ufafanuzi kuhusu hatua dhidi ya Msambatavangu, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (Siasa na Uhusiano wa Kimataifa), Kanali Ngemela Lubinga alisema mwanachama anapovunja miiko ya chama na kusimamishwa au kufukuzwa, kuna hatua zinazompasa kuzifuata kabla ya kurudishwa.

Alisema moja ya hatua hizo ni kuomba kurudi kwa kukubali kosa au kukataa kwa kujitetea, kisha barua ya maombi kupokewa na kupelekwa kwenye kamati ya maadili na usalama ambako hujadiliwa na kupelekwa NEC.

“Inawezekana huko kote wajumbe wasikubaliane na utetezi wako kulingana na miiko uliyokiuka, hivyo watakusimamisha kwa kipindi kisichokuwa na ukomo ambacho ni cha kukuangalia kama uliyoyakataa ulionewa au uliyoyakubali umeyaacha kweli au ni utapeli,” alisema.

“Katika kipindi hicho cha kusimamishwa kwa muda usio na ukomo unaweza kuitwa baada ya kujiridhisha kuwa umeacha uliyokiri au unaweza usiitwe na ukalazimika kuandika barua ya kuomba tena, kimsingi ni kujiridhisha na mabadiliko ya tabia yako kama unafaa kuwa mwanachama wa CCM mwadilifu kama inavyoelekeza miiko ya chama.”

Nyongeza na Kalunde Jamal



Chanzo: mwananchi.co.tz