Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msajili wa Vyama aukimbia mgogoro NCCR-Mageuzi

Mutungi Pic Data Msajili wa Vyama aukimbia mgogoro NCCR-Mageuzi

Wed, 20 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati mvutano ukiendelea kushika kasi ndani ya Chama cha NCCR- Mageuzi, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amesema ofisi yake imejitoa katika kusuluhisha mgogoro huo kwa sababu mbili, ikiwemo kuheshimu katiba ya chama hicho.

Akizungumza Dar es Salaam, Jaji Mutungi alisema kwa kile kinachoendelea ndani ya chama hicho ameona bora aheshimu matakwa ya katiba yao ili waendelee kuushughulikia kupitia vikao vya ndani ya chama.

“Kwenye ofisi yangu hakuna lolote mbali na kuahirisha hiyo kesi yao, na kwa kile kinachoendelea ndani ya chama hicho tumeona tujiondoe na tuheshimu katiba yao na kwa hatua iliyofiki acha tuone wao watafikia wapi…lakini wakiendelea kuzozana tutaingilia tena,” alisema.

Jaji Mutungi alifafanua sababu ya kuahirisha kikao cha upatanishi Juni 21 mwaka huu, kuwa ni kutokana na Mwenyekiti wa chama hicho James Mbatia kuandika barua kwenda kwa waziri na kwamba, aliheshimu maamuzi hayo ya upande mmoja hadi yapatiwe majibu.

“Naheshimu maamuzi yaliyotolewa na upande mmoja na tumeona tujipe muda hadi hapo waziri atakapowajibu kwa hiyo sisi (Ofisi ya Msajili) hatuna lolote zaidi ya kuahirisha kesi yao,’’ alisema Jaji Mutungi

Jaji Mutungi ametoa ufafanuzi huo baada ya juzi Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Martha Chiomba kutoa tamko akiweka msisitizo kwamba Mbatia hapaswi kujihusisha na jambo lolote linalohusiana na chama hicho hadi atakapoenda kujitetea kwenye mkutano mkuu kulingana na tuhuma zinazomkabili.

Advertisement “Nataka wanachama wajue kwamba Mbatia na wenzake walisimamishwa sababu za kufikia uamuzi huo walishaandikiwa na hatakiwi kujihusisha na lolote hata kutumia nembo za chama na hatakiwa kufanya mikutano na kutumia majengo ya chama chetu hadi atakapokuja kujitetea kwenye mkutano mkuu,’’ alisema Chiomba.

Chiomba alisema wanashangaa kiongozi huyo na kundi lake bado wanaendelea kujihusisha na shughuli za chama hicho licha ya kwamba walishapewa barua ya kusimamishwa hivyo uongozi uliopo madarakani unasikitishwa na kitendo cha Mbatia kudharau maamuzi ya vikao halali.

Wakati Chiomba akitoa msimamo huo, Mbatia alisema hawezi kujibu anachoeleza Jaji Mutungikwa sababu ofisi yake ilijiingiza katika mgogoro kuleta utata.

“Alichosema Jaji Mutungi ni NCCR ifuate katiba yake ni sahihi kabisa sasa inafuataje katiba wakati tatizo lilipojitokeza ofisi yake ilijiingiza na kuleta utata kwenye katiba ya chama,’’ alisema

Alisema wamemwandikia waziri kumwomba alisimamia suala hilo kiutawala. “Tulimwomba amuelekeze msajili vizuri namna ya kusimamia sheria na mimi naamini kwenye taratibu zaidi na naomba zifuatwe ili chama chetu kiifanye Tanzania kuwa sehemu salama ya kuishi,’’ alisema Mbatia.

Jitihada za gazeti hili kumpata Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene na Katibu Mkuu, Dk John Jingu kujua suala hilo lilipofikia hazikusaa matunda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live