Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msajili atoa neno vyama kushirikiana

66196 Pic+mutungi Msajili atoa neno vyama kushirikiana

Mon, 22 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa, imesema vyama ambavyo vinataka kushirikiana kwenye uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu vimeshachelewa kwa mujibu wa sheria.

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, aliyasema hayo jana katika mahojiano maalum yaliyolenga kujua msimamo wa ofisi hiyo, kuhusu suala la ushirikiano wa vyama vya siasa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Akijibu kuhusu suala hilo, Nyahoza alisema mpaka sasa ofisi yake haijapokea mkataba wa makubaliano ya ushirikiano kutoka kwa chama chochote cha siasa.

Hivyo, alisema kwa mujibu wa sheria vyama ambavyo vina nia ya kushirikiana vimeshachelewa.

“Ipo sheria iliyoainishwa kwenye Kifungu namba 11 (a) cha sheria hivyo kama vyama havitaifuata vitakuwa vimeivunja. Vyama vya siasa vinavyotaka kushirikiana bila kufuata sheria hii vitakuwa vimeivunja.

Alifafanua kuwa, ushirikiano wa vyama umeratibiwa vizuri kisheria ambapo vyama vinapohitaji kushirikiana vinapaswa kutumia vikao halali vya chama badala ya utashi wa mtu binafsi.

“Baada ya vikao halali kupitisha azimio la kufanya ushirikiano, vyama husika vinapaswa kuwasilisha mkataba wa ushirikiano katika ofisi ya msajili ofisi miezi mitatu kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza,” alisema.

Alisema vyama havijakatazwa kushirikiana bali vimewekewa utaratibu ili Tume ya Uchaguzi pamoja na taasisi zote zinazohusika ziweze kujiandaa vizuri na kuimarisha ulinzi hasa wakati wa kampeni.

Pia, alisema lengo lingine ni kuvisaidia vyama vingine kuelewa wanashindana na chama gani.

Alisema hadi sasa vyama vyenye usajili wa kudumu ni 19 na kimoja kina usajili wa muda, na maombi ya vyama 16 bado yanafanyiwa upembuzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live