Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msajili apokea mapendekezo ya katiba mpya, tume huru

Katibapic Data 1140x640 Msajili apokea mapendekezo ya katiba mpya, tume huru

Wed, 19 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema imepokea mapendekezo yaliyotolewa na wadau wa vyama vya siasa nchini ukiwamo mchakato wa katiba mpya.

Mapendekezo mengine ni serikali kuwaandalia ziara za nje ya nchi viongozi wa kisiasa kwa lengo la kujifunza na uwekwaji wa mfumo wa uchaguzi huru na haki kwa mwaka 2025.

Akizungumza wakati akifunga mkutano wa siku mbili wa viongozi wa vyama vya siasa Dar es Salaam jana, Naibu Msajili wa vyama vya siasa nchini, Mohhamed Ali alisema kupitia mkutano huo, wamepata fursa ya kuelewa namna ya kuboresha vyama na kukuza demokrasia.

“Tunampongeza Rais (Samia Suluhu Hassan) aliona kuna wajibu kila Mtanzania kuwa na fursa ya kuchangia demokrasia katika nchi kwa kushirikisha wanasiasa wote, wanajamii, wanataaluma na wengine na nia ya Rais kusikilizana na kuvumiliana ili kujenga taifa la kuheshimiana,” alisema Ali.

Aliongeza: “Tanzania ni yetu sote, haijalishi unatoa maoni yako ukiwa na sauti kali na ya utaratibu, tutajali kilichomo katika uwasilisho, maoni yote tutachukua na kuijenga Tanzania yenye demokrasia pana.”

Kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alipendekeza kuundwa kamati na watu ambao watakuwa wajumbe wa kamati ya tume hiyo. “Pendekezo letu ni uchaguzi wa serikali za mtaa uweze kusimamiwa na tume huru ya uchaguzi lakini hilo halijafanyika na kwa muda uliopo haliwezi kufanyika sasa, uchaguzi ulio huru na haki ni mtihani,” alisema Profesa Lipumba.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AFP), Said Sudi alisema demokrasia ni pamoja na kuchukua viongozi wa vyama vya siasa kwenda kujifunza siasa za nchi nyingine. “Viongozi wa kisiasa wakajifunza namna ya kutunza amani…kuna vyama 19 na pesa ya Watanzania zitumike kwa wote na hizo ziara zake (Rais Samia) abebe viongozi wa kisiasa na raia wachache lazima waende wakajifunze,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohammed alisema muda uliobaki hautoshi kwa kuandaa katiba mpya kwani ni zoezi ambalo linachukua muda ikiwamo kukusanya maoni ya wananchi, hivyo sio kitu cha muda mfupi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live