Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msajili apokea maombi 16 ya vyama vipya vya siasa

683820e10e231dfb9a5d2f0519f85542.jpeg Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa

Tue, 2 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema hadi sasa wamepokea maombi 16 ya usajili wa vyama vya siasa.

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, Jaji Mutungi alisema tofauti na maombi ya vyama vingine, ombi la kusajiliwa Chama Cha Umoja lilitangazwa kwenye gazeti ili kutekeleza marekebisho ya Sheria ya Vyama vya siasa ya mwaka 2019 na kanuni zake.

Alisema vyama vingine vilivyotuma maombi havikutangazwa kwa sababu sheria iliyokuwepo haikuagiza hilo lifanyike.

“Kutangazwa kwa kusajiliwa kwa chama hiki haimaanishi kimeshasajiliwa hapana, hii ni hatua ya awali kabisa wala hakina hata usajili wa muda. Na hatua hii ya kutangaza kwa sasa ni ya lazima kisheria,” alisema Jaji Mutungi.

Ofisi hiyo ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilitangaza gazetini kuwepo ombi la kusajiliwa chama kitakachoitwa Chama cha Umoja na kueleza kuwa endapo kuna mtu ana pingamizi na jina, alama, rangi ya chama hicho au jambo lolote kuhusu usajili wa chama hicho atoe taarifa.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, mtu mwenye pingamizi anapaswa kuwasilisha pingamizi hilo katika ofisi ya msajili ndani ya siku 21 tangu tarehe ya tangazo hilo.

Kwa sasa Ofisi hiyo imetoa usajili wa kudumu kwa vyama 19 ambavyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Democrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha NCCR-Mageuzi, Union for Multiparty Democracy (UMD) na National League for Democracy (NLD).

Vyama vingine ni ​United Peoples’ Democratic (UPDP),National Reconstruction Alliance (NRA), African Democratic Alliance (ADA-TADEA)Tanzania Labour (TLP),United Democratic Party (UDP), Demokrasia Makini (MAKINI), Democratic Party (DP), Sauti ya Umma (SAU),​ Alliance for African Farmers Party (AAFP) na Chama cha Kijamii (CCK).

Pia, vyama vingine vyenye usajili wa kudumu ni Alliance for Democratic Change (ADC), Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) na Chama cha ACT-Wazalendo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz