Dar es Salaam. Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania amekiandikia barua Chadema kukitaka kuwasilisha ratiba ya mkutano mkuu wa kuchagua viongozi wa kitaifa wa chama hicho kabla ya Novemba 11, 2019.
Barua hiyo imetolewa leo Jumatano Novemba 6, 2019 na naibu msajili wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza kwa niaba ya msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi.
Oktoba Mosi, 2019 chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania kiliandikiwa barua na ofisi hiyo wajieleze kwanini wasichukuliwe hatua kwa madai ya kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa kwa kuchelewa kufanya uchaguzi mkuu wa chama hicho.
Chama hicho kilijibu barua hiyo ya msajili kwa hoja sita.
Katika barua hiyo msajili amesema lengo la kutaka maelezo hayo ni kurahisisha ofisi ya msajili kutekeleza majukumu yake.
“Pamoja na mambo mengine, ratiba hiyo ionyeshe tarehe ya kutoa fomu za kugombea kwa wanachama wenye nia ya kugombea, tarehe ya uteuzi wa wagombea na uchaguzi.”
Pia Soma
- Serikali yakiri bangi tatizo kubwa
- Mbunge achomwa kisu
- Polisi bado wanachunguza sakata la Idris Sultan
Nyahoza alipoulizwa kuhusu barua hiyo amesema imetolewa na ofisi ya msajili, kwamba ni mwendelezo wa barua ya Oktoba Mosi, 2019.
Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amelieleza Mwananchi kuwa hajapata barua hiyo, “nipo katika kikao sijaiona barua yenye maudhui hayo.”
Kifungu cha 4 (5) (b) cha Sheria ya Vyama vya Siasa sura ya 258 (RE.2019) kinaipa ofisi hiyo mamlaka ya kufatilia uchaguzi na uteuzi wa viongozi wa vyama vya siasa ili kuhakikisha unafanyika kwa mujibu wa sheria hiyo, katiba na kanuni za chama husika.