Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekiri kupokea barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, inayowataka wajielezea ndani ya siku tano, tangu kupokea barua hiyo.
Kwa kujibu wa barua hiyo ambayo bado haijawekwa hadharani ilipokelewa na chama hicho tangu Oktoba 2, 2023 mchana, kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ikitaka wajielezea kwa madai ya kurekodi maudhui ya video ya kumdhalilisha Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
CCM inakishutumu chama hicho cha upinzani, ikidai kimerekodi maudhui ya video hiyo na kuyasambaza kwenye mitandao yake ya kijamii, pamoja na ya wafuasi wake, maudhui ambayo yanaashiria kutengenezwa kwa makusudi kwa lengo la kutaka kumshushia hadhi kiongozi wao.
Mwananchi Digital ilipomuuliza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuhusu barua hiyo, amekiri ni kweli japo aligoma kufafanua kwa madai yupo likizo.
"Siwezi kulifanunua jambo hili kwa undani niko likizo," amesema.
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amekana chama hicho kuhusika na suala hilo huku akieleza hata mitandao ya chama hicho haijarekodi taarifa zinazoelezwa kupitia barua ya msajili.
"Toka nilipopokea barua hiyo Oktoba 2, 2023 nimepitia mitandao rasmi ya kijamii ya Chadema sijaona video hiyo. Nafahamu pia Chadema haijatengeneza video yenye maudhui kama hayo yanayolalamikiwa," amesema Mnyika.
Mnyika amedai Ofisi ya Msajili inaendelea kupokea malalamiko hayo kutokana na kanuni kandamizi za maadili ya vyama vya siasa za mwaka 2019 zilizotokana na marekebisho mabaya ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019.
"Tunaendelea kutaka Katiba Mpya itakayowezesha kuwa na taasisi huru ikiwamo ofisi huru ya Msajili wa Vyama na kutungwa kwa sheria mpya ya vyama itakayolinda demokrasia, uhuru na haki za vyama vyama vya siasa," amesema.