Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msajili aanza kutembelea ofisi za vyama, aionya AAFP

Vyama Pc Data Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini

Tue, 31 Aug 2021 Chanzo: MWANANCHI

Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini, imetoa wiki moja kwa Chama cha Wakulima cha AAFP kukamilisha kanuni zilizowekwa pamoja na kurekebisha mfumo mbovu wa matumizi ya fedha.

Agizo hilo limetolewa leo Agosti 30, na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza wakati wa zoezi la uhakiki wa vyama hivyo ambalo liameanza leo kwa chama hicho na Chama cha NRA.

Zoezi la uhakiki wa vyama vya siasa ni takwa la kisheria kuhakikisha vyama 19 vyenye usajili kamili vinatekeleza masharti ya usajili kama yalivyoainishwa kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa na kanuni zake.

Akizungumza mara baada ya uhakiki huo, amesema wamegundua chama hicho bado kina mapungufu mengi hivyo, ametoa wiki hiyo moja ili waweze kukamilisha mapungufu hayo.

"Mambo mengi hawajakidhi, tumeona pia kuna mfumo mbovu wa matumizi ya fedha, kwahiyo tunatoa wiki moja wakamilishe na baada ya muda huo tulioutoa tutarudi tena kuangalia," amesema Nyahoza.

Naye Katibu wa AAFP, Rashid Ally amesema ameyapokea maelekezo hayo na kuahidi atayafanyia kazi huku akiitaka ofisi hiyo iweze kuzungumza na serikali ili waruhusiwe kufanya mikutano ya kisiasa

"Ofisi ya Msajili isiishie tu kuvibana vyama vya siasa waongee na serikali ili turuhusiwe kufanya mikutano. Mikutano ndo inatusaidia katika kuimarisha chama, sasa utasemaje kama una chama wakati huruhusiwi kufanya mikutano ya kisiasa, hata mkisema mkae vikao vya ndani mnakamatwa," amesema Ally.

Zoezi hilo litaendelea kesho kwa kuhakiki vyama vya UDP na NLD, vikifuatiwa na vyama vya UMD na ADC, Septemba 1, 2021.

Mbali na vyama hivyo, Septemba 2 vyama vya CCK na Demokrasia Makini vitafanyiwa uhakiki na Septemba 3 itakuwa zamu ya chama cha Chadema na UPDP.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo uhakiki utaendelea wiki inayoanza Septemba 6 kwa kuhakiki vyama vya NCCR na Chaumma. Vyama vingine vitakavyohakikiwa wiki hiyo ni pamoja na vyama vya ACT-Wazalendo, CUF, TLP, SAU, ADA TADEA na DP huku uhakiki wa CCM ukitarajiwa kufanyika makao makuu ya chama hicho mkoani Dodoma Septemba 10, 2021.

Baada ya kuhakiki ofisi za Dar-es-salaam na Dodoma, uhakiki huo utahamia ofisi za Zanzibar kuanzia Septemba 13 kwa kuhakiki vyama vya AAFP na NRA.

Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa kila chama chenye usajili kamili kinatakiwa kuwa na ofisi pande zote mbili za Muungano.

Chanzo: MWANANCHI