Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msajili aagiza CUF kujibu malalamiko ya waliotimuliwa

CUF Msajili aitaka CUF kujibu malalamiko ya waliotimuliwa

Tue, 30 Nov 2021 Chanzo: ippmedia.com

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeuandikia barua uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), ikiutaka kujibu malalamiko yaliyofikishwa kwenye ofisi hiyo na wanachama wanaodai kuvuliwa uongozi na kufukuzwa katika chama.

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisthy Nyahoza, aliliambia gazeti hili jana kuwa ofisi yake inasubiri majibu kutoka katika uongozi wa chama hicho ili iweze kutoa uamuzi wa malalamiko hayo.

"Tuliwapelekea barua hiyo Novemva 26 mwaka huu na wanatakiwa kufikia Ijumaa ya wiki hii wawe wameijibu, ili hatua nyingine za kushughulikia malalalamiko hayo ziendelee kuchukuliwa," alisema Nyahoza.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Magdalena Sakaya, alithibitisha kupokelewa kwa barua hiyo, na kwamba itafanyiwa kazi baada ya kuangalia kile ambacho Ofisi ya Msajili inataka kujibiwa.

"Sipo ofisini, lakini nimepata taarifa za kuwapo kwa barua hiyo, lakini sijajua ni nini kinatakiwa kujibiwa, hivyo viongozi wa CUF tutawasiliana ili kuangalia ni nani wanatakiwa kujibu na nini kinatakiwa kujibiwa," alisema Sakaya.

Alifafanua kuwa inawezekana ni barua inayotakiwa kujibiwa na kiongozi, mmoja au baraza, na kwamba watakapoisoma ndipo watajua imeelekezwa kwa nani, ili ijibiwe haraka iwezekanavyo.

Hivi karibuni, baadhi ya wanachama wa CUF waliwasilisha malalamiko yao katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, jijini Dodoma, wakipinga kuondolewa katika chama hicho wakidai kuwa taratibu hazikufuatwa.

Miongoni mwao ni aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Uhusiano na Umma wa CUF, Abdul Kambaya wakiwamo pia Ahmed Hamis, Mohamed Vuai, Ali Makame na Mtumwa Ambari.

Wengine waliofukuzwa na Baraza Kuu la CUF chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba ni Ahmed Hamis, Mohamed Vuai, Ali Makame, Mtumwa Ambari, Hamida Huweshi na Dhifaa Mohamed Bakari.

Aidha, wanachama hao ambao inaelezwa kuwa walikuwa ni wajumbe wa baraza hilo pia yumo Chande Jidawi aliyekuwa Kaimu Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa chama hicho.

Chanzo: ippmedia.com