Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mrema aidai fidia Serikali ya Tanzania Sh2 bilioni

91213 Pic+mrema Mrema aidai fidia Serikali ya Tanzania Sh2 bilioni

Thu, 9 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Mwenyekiti taifa wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema ameitaka Serikali ya Tanzania kumlipa Sh2 bilioni kama fidia ya kesi alizowahi  kusingiziwa chini ya Serikali ya awamu ya tatu ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Mbali na fidia pia amemuandikia barua Rais wa Tanzania, John Magufuli iliyo na malalamiko yake na kuomba kukutana naye ili waweze kuzungumza juu ya yale aliyofanyiwa na serikali.

Mrema ameyasema hayo leo Jumatano Januari 8, 2020 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya TLP, Magomeni jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia hali ya kisiasa nchini tangu awamu ya tatu hadi sasa.

Amesema kwa nyakati tofauti ndani ya uongozi wa Rais Mkapa alisingiziwa kesi ikiwamo ya kumhusisha Rais huyo na rushwa ya Sh500 milioni akiwa katika kampeni za kugombea ubunge wa Temeke mwaka 1996, kutengeneza nyaraka mbalimbali zilizohusisha viongozi wa serikali na tuhuma za rushwa pamoja na kutumia ushahidi wa uongo kushinda kesi.

Amesema kwa sababu Serikali imesema kumbambikia kesi mtu  ni kosa la jinai ambapo wahusika wanatakiwa kukamatwa na kufikishwa mahakamani lakini muathirika anatakiwa kulipwa fidia ameomba Rais Magufuli kumlipa fidia kwa niaba ya serikali.

“Kwa kuwa nilibambikiwa na kuzushiwa ya uongo ambayo ni kosa kisheria, nakuomba Rais wa Tanzania (John Magufuli) na serikali yako inilipe Sh2 bilioni kwani haya yote yalifanyika ili kukisaidia chama tawala na serikali yake ili kinishinde kisiasa,” amesema Mrema

“Hiyo hela ni ya chumvi na wasiponifidia nitawashtaki kwa wananchi na ninamuomba Rais Magufuli afute historia ya kuonewa kwa watu nchini na kuonewa kwangu,” amesema

Amesema kitendo cha  kupewa kesi za uongo kulimuathiri kisaikolojia kwani jamii iliyokuwa ikimzunguka ilimuona kama mtu mwovu kutokana na kukamatwa na polisi kila mara.

“Sioni unafuu katika kunyamaza kwa sababu nchi hii ukiwa na nguvu wanaangalia namna ya kukudhoofisha kwa kutumia mbinu tofauti na hila kwa kutumia vyombo vyao,” amesema Mrema

“Mengine nimevumilia sana mpaka basi, wapo wengine wanasema hakuna wa kuiondoa CCM madarakani ni kweli, inaondokaje kwa udhalimu huu na mtaji iliyonayo,” amesema Mrema

Chanzo: mwananchi.co.tz