Huenda jina la Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), likajulikana muda wowote kuanzia sasa wakati kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC) kikitarajiwa kuketi ndani ya siku tatu kuanzia leo Jumamosi, Januari 13, 2024 Unguja, Zanzibar chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kiti hicho kipo wazi tangu Novemba 27, 2023 baada ya aliyekuwa akikishikilia, Daniel Chongolo kujiuzulu kutokana na kuhusishwa na tuhuma mbalimbali na nafasi yake hivi sasa inakaimiwa na Anamringi Macha ambaye ni Naibu Katibu Mkuu (Bara).
Macha anatekeleza wajibu huo ikiwa pia anaendelea na majukumu yake jambo linalowafanya baadhi ya makada wa chama hicho kuona ana mzigo mzito hali inayoweza kupunguza ufanisi wa anachokifanya.
Kikao cha NEC kitakachofanyika visiwani humo kinaweza kutoka na jina la mrithi wa Chongolo kwa kuwa kisipofanya hivyo kitalazimika kukutana tena kwa dharula kufanya jukumu hilo hali inayoelezwa itaongeza gharama zaidi kwa chama.
Ibara ya 115, 7(a hadi d) inaeleza Katibu Mkuu wa CCM atakuwa na majukumu ya kuratibu kazi zote za chama hicho, kusimamia kazi zote za utawala na uendeshaji, kufuatilia na kuratibu masuala ya usalama na maadili katika chama na kusimamia udhibiti wa fedha na mali za chama hicho.
Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Bara, ndiye atakayekuwa msaidizi mkuu wa Katibu Mkuu na atafanya kazi zozote za chama hicho atakazopangiwa na kiongozi wake huyo.
Katika mazingira ya sasa ambayo CCM kinajiandaa kwa ajili ya uchaguzi za serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu, baadhi ya makada wa chama hicho wanaona ni wakati mwafaka akapatikana katibu mkuu atakayeongoza mikakati ya ushindi kwenye uchaguzi huo.
Makada hao wanaona mwaka huu utakuwa na mambo mazito ikiwemo Bunge la Bajeti ambalo litakuwa na bajeti ya uchaguzi wa serikali za mitaa lakini wakati huohuo akili zikiwaza pia Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwakani.
Kutokana na mazingira hayo, kiti cha Katibu Mkuu kuendelea kuwa wazi hakitoi ishara nzuri katika uendeshaji wa shughuli za kila siku hivyo NEC inaweza kuidhinisha jina litakalopelekwa kwao na Mwenyekiti wake.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, ibara ya 101 (2) inasema Halmashauri Kuu ya CCM Taifa itafanya mikutano yake ya kawaida mara moja katika kila baada ya miezi sita.
Lakini, inaweza kufanya mkutano usiokuwa wa kawaida wakati wowote endapo itatokea haja ya kufanya hivyo au kwa maagizo ya kikao cha juu.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa chama hicho ana uwezo wa kuitisha kikao hicho kwa dharura kama kuna jambo analohitaji lipate idhini ya wajumbe.
Akizungumza na Mwananchi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mohamed Ali Kawaida amesema kila kikao kinachofanyika kimo ndani ya katiba na vikao vya NEC hufanyika kila baada ya miezi sita.
Kuhusu NEC ya dharura, Kawaida ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ameeleza ni Mwenyekiti wa chama hicho ndiye anayeamua kuhusu sababu za kuitisha kikao hicho kwa dharura.
“Huwa sababu anayejua ni Mwenyekiti, akiona kuna haja ya kuitisha NEC ya dharura anaitisha na mnaarifiwa kwa ajili ya kushiriki. Lakini ni vigumu kujua sababu fulani inaweza kuitisha NEC ya dharura Mwenyekiti ndiye anayeamua,” amesema.
NEC ya dharura
Oktoba 22, 2023 Rais Samia aliitisha kikao cha dharura cha NEC kilichofanyika mkoani Dodoma ambacho pamoja na mambo mengine kiliidhinisha jina la Paul Makonda kuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi.
Kuidhinishwa kwa Makonda kulikuja siku moja baada ya aliyekuwa akishikilia wadhifa huo, Sophia Mjema kuteuliwa kuwa Mshauri wa Rais kwenye masuala ya wanawake na makundi maalumu, Oktoba 21, 2023.
Mwezi mmoja baadaye, (Novemba 29, 2023), kikao cha NEC kilifanyika jijini Dar es Salam chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia, ambaye aliridhia ombi la Chongolo kujiuzulu kwa madai ya kuchafuliwa katika mitandao ya kijamii.
Katika barua hiyo ya Novemba 27, 2023 iliyosambaa mitandaoni, Chongolo alikaririwa akisema hali hiyo imemkumbusha wajibu wa kiongozi kuwajibika kwa masilahi ya chama wakati wote anapotuhumiwa au kuhusishwa na jambo lolote.
Rais Samia aliridhia ombi la kujiuzulu kwa Chongolo aliyehudumu nafasi hiyo kwa siku 942, tangu alipochaguliwa na NEC Aprili 30, 2021 akirithi mikoba ya mtangulizi wake, Dk Bashiru ambaye hivi sasa ni mbunge wa kuteuliwa.
Macho, masikia Zanzibar
Wakati Watanzania na wana-CCM wakiwa na shauku ya kutaka kujua mrithi wa Chongolo au kama mtendaji huyo atarejeshwa katika wadhifa wake, chama hicho tawala kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) kimetoa tangazo linaloashiria uwepo wa vikao kikiwakaribisha wajumbe wote wa halmashauri kuu visiwani Zanzibar.
“Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kikiongozwa na mwenyekiti wake, Samia Suluhu Hassan na Makamu mwenyekiti, Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi, kinawakaribisha wajumbe wote wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kisiwani Zanzibar.
“Mnakaribishwa kushiriki madhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yatakayofanyika Januari 12, 2024 (jana). Pia, mnakaribishwa kwa vikao vya kuendelea kujenga chama chetu cha Mapinduzi.”
Mwananchi lilipomtafuta Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Macha kuzungumzia kuhusu vikao hivyo, alimtaka mwandishi amtafute Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda.
“Kuhusu masuala yote yanayohusu taarifa kwa vyombo vya habari, nakuomba uwasiliane na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM (Paul Makonda),” amejibu Macha kupitia ujumbe mfupi.
Hata hivyo, Makonda alipotafutwa na gazeti hili kwa simu zake za mkononi hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kujua undani wa vikao hivyo hakujibu.
CCM bila mtendaji mkuu
Vikao hivyo vinafanyika wakati huu ambao CCM haina mtendaji mkuu wa chama na ukizingatia mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
Taarifa kutoka ndani ya CCM zinaeleza, suala la katibu mkuu limekuwa na vuta nikuvute kutoka kwa makada mbalimbali hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na baada ya hapo.
“Unajua katibu mkuu ndio injini ya chama, sasa hata wana mtandao wa urais 2025 na hata 2030 watataka katibu mkuu wao, kwa hiyo hii si vita ndogo. Mambo magumu kwelikweli, lakini wacha tusubiri kuona,” amedokeza kada mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake na kuongeza:
“Ngoja tusuburi kuona, inawezekana Chongolo akarudishwa au akapatikana mwingine. Lolote linawezekana.”
Makada wanaotajwa kumrithi Chongolo
Mwananchi limedokezwa kuwa vita ya kusaka nafasi ya kumrithi Chongolo sio ndogo na imekuwa ikipiganwa chini kwa chini baadhi ya makada na wapambe wao kujaribu kuonyesha ushawishi.
Kabla hata ya Chongolo kujiuzulu wadhifa huo, wingu na shauku ya baadhi ya makada kutabiri ama kujaribu kushawishi mabadiliko lilikuwa likitikisa ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, mara kadhaa wakati vikao vya juu vya chama vilipokuwa vikikaribia hoja za chini kwa chini zilikuwa zikisikika hadi kwenye mitandao ya kijamii, lakini mara zote Chongolo alibaki salama.
Katika vuguvugu hilo kumekuwa na majina kadhaa ambayo yanachomoza kukalia kiti hicho akiwemo waziri wa zamani katika Serikali ya awamu ya nne, Balozi Emmanuel Nchimbi, wakuu wa mikoa, Amos Makalla (Mwanza) na Martin Shigella (Geita).
Pia, wamo washauri wa Rais (Siasa na Uhusiano wa Jamii), Abdallah Bulembo aliyewahi pia kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi na William Lukuvi, ambaye pia ni mbunge wa Ismani na waziri mwandamizi mstaafu pamoja na Anthony Mtaka (mkuu wa mkoa Njombe) nalo limekuwa likichomoza.
Kibarua Katibu mkuu ajaye
Kwa hali ilivyo, mbali ya majukumu ya kikatiba, Mwananchi linatambua kuwa mtendaji ajaye, atakuwa na kibarua cha kukiuhisha chama kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kuratibu mchakato wa Ilani ya uchaguzi wa CCM ya mwaka 2025/30.
Majukumu mengine ni kudhibiti ukuaji wa makundi ndani ya chama hicho yanayopigana vikumbo kupanga safu za viongozi kuelekea katika chaguzi zijazo.
Pia, atakuwa na kibarua cha kuhakikisha anashindana kwa hoja na wapinzani waliobeba ajenda ya ugumu wa maisha, Katiba Mpya na maboresho ya miswada sheria ya uchaguzi na vyama vya siasa.
Baadhi ya wachambuzi wa siasa, walisema ingawa ajenda ya vikao hivyo havijawekwa wazi, huenda suala la kumpata katibu mkuu mpya likajadiliwa na kuthibitishwa.
“Kuna tangazo la CCM limeliona mtandaoni linasema wajumbe wote wa halmashauri kuu waende Zanzibar kuhudhuria mapinduzi, kisha kushiriki vikao vya chama, sasa unaposema kujenga chama si pamoja na kuwa na mtendaji mkuu wa chama?
“Kutokuwa na mtendaji mkuu wa chama tangu mwaka 2023 hadi leo sio afya, yeye ndio kila kitu ni kiongozi anayetakiwa kuwepo, huenda ajenda hii ikajadiliwa,” amesema Dk Aviti Mushi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Dk Mushi amesema kuna watu wengi wanaotajwa tajwa kumrithi Chongolo, lakini yeye anafikiri huenda Balozi Nchimbi akachukua nafasi hiyo, ingawa CCM ni chama kikubwa chenye hazina ya watu wengi.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa Zanzibar, Ali Makame Issa, amesema katika vikao hivyo kuna mambo matatu yanaweza kujadiliwa ambayo suala la kumteua na kumthibitisha katibu mkuu, watendaji wa Serikali wasioendana na kasi ya Rais Samia, miswada mitatu ya sheria ya uchaguzi na sheria vya siasa ya mwaka 2023 iliyowasilishwa bungeni mwaka jana.
“Kwa hatua tuliyoifikia sasa na kuelekea katika chaguzi za Serikali za mitaa, ni vigumu chama kukaa bila katibu mkuu, inawezekana vikao hivyo vikafanya uamuzi nani atakuwa katibu mkuu pamoja na kupanga mikakati kuhusu miswada ya sheria ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa,’’ amesema na kuongeza:
“Miswada hii ni moja ya mambo ambayo huenda CCM wakajadili ili kuweka msimamo kama chama utakaodumu kutokana na mapendekezo ya wadau wa demokrasia kuhusu sheria hizo.
Hata hivyo, Issa hakutaka kuweka wazi makada wanaotajwa kuwania kiti cha Chongolo, akisema CCM ina hazina ya watu ambao wakipewa nafasi wanaweza kuwa bora katika utekelezaji wa majukumu yao.