Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Monduli wamkaribisha Lowassa kurejesha umoja uliotoweka

44835 Pic+luwasa Monduli wamkaribisha Lowassa kurejesha umoja uliotoweka

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mbunge wa Monduli (CCM), Julius Kalanga amesema wameshukuru sana, uamuzi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kurejea CCM kwani sasa atasaidia kurejesha mshikamano wa wananchi wa wilaya hiyo uliokuwa umetoweka na hivyo kusukuma mbele maendeleo ya wilaya ya Monduli.

Akizungumza jana na Mwananchi Kalanga alisema tangu Lowassa ajiondoe CCM Julai 28, 2015 na kujiunga na upinzani, kulikuwepo mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wakazi wa wilaya hiyo na hivyo kuchangia kuzorotesha maendeleo lakini sasa kurejea kwake ni faraja kwa wana-Monduli ambao kihistoria ni wana-CCM.

"Tunampongeza kwa kufanya uamuzi wake na kurejea CCM, Lowassa ana mchango mkubwa wa maendeleo katika jimbo la Monduli na sasa tuendelee kushirikiana naye kuenzi mambo yote aliyoyafanya alipokuwa mbunge," alisema.

Lowassa alikuwa mbunge wa Monduli kupitia CCM kwa miaka 25 na kabla ya hapo, alikuwa mbunge wa chama hicho kupitia kundi la vijana.

Kalanga alisema Monduli kulikuwa na mgawanyiko mkubwa ambao, ulikuwa hauna maana na sasa kurejea kwake kutaimarisha mahusiano baina ya wananchi na hivyo kuchochea maendeleo.

Soma Zaidi: Lowassa arejea CCM, asindikizwa na Rostam

Katika hatua nyingine, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, Loota Sanare alisema CCM Arusha inamkaribisha Lowassa nyumbani na inaamini alikuwa safarini sasa amerejea nyumbani.

"Tunamkaribisha Arusha aje tufanyekazi ya kumuunga mkono, Rais John Magufuli katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi wa CCM," alisema.

Sanare alisema CCM mkoa wa Arusha, itashirikiana na Lowassa katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, kuhakikisha CCM inashinda viti vyote mkoani Arusha.

Soma Zaidi: Selasini: Lowassa katuacha kama alivyotukuta

Hata hivyo, mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, Aman Golugwa, alisema Chadema bado ipo imara licha ya Lowassa kurejea CCM.

"Mapambano bado yanaendelea Mzee Lowassa ameishiwa pumzi kama unavyojua siasa za kuwa upinzani ni mapambano, kama ambavyo Rais alisema alikuwa anamuona anateseka, hatujui mateso gani, lakini sisi tupo Imara kama alivyotukuta na tutaendelea kufanya vizuri," alisema.

Golugwa alisema Lowassa alichangia kiasi chake katika harakati za mageuzi nchini na alipoishia ni uhuru wake lakini, kurejea CCM kwa Arusha, wasitambe kuwa watashinda majimbo tuliyochukua mwaka 2015 na viti vya Serikali za mitaaa.

Soma Zaidi: Wapinzani watema nyongo Lowassa kuhama wamchambua

 



Chanzo: mwananchi.co.tz