Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mnyika ataja chanzo kifo cha muasisi wa Chadema, aliificha familia

Muasisi Cdm.jpeg Mnyika ataja chanzo kifo cha muasisi wa Chadema, aliificha familia

Sat, 18 Mar 2023 Chanzo: Mwananchi

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika ameongoza mamia ya wanachama wa Chadema na ndugu kuaga mwili wa Sylvester Masinde (82) nyumbani kwake Mtaa wa Susuni Kata ya Mahina jijini Mwanza, huku Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe akitarajiwa kuongoza shughuli ya kuaga mwili huo kanisani.

Mzee Masinde ambaye mbali na kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya chama hicho, pia ni miongoni mwa waasisi wa chama hicho alifariki Machi 15 mwaka huu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando alipokuwa akipatiwa matibabu.

Akitoa salamu za rambirambi mbele ya familia ya marehemu, Mnyika amesema Masinde alifariki kwa ugonjwa wa saratani ya tezi dume aliougua kwa miaka mingi.

Mnyika amesema mzee Masinde pamoja na kutambua kuwa anaumwa ugonjwa huo lakini hakutaka ufahamike kwa familia na ndugu wa karibu ili kutozua taharuki na kuwafanya wakate tamaa.

"Wakati wote akiwa ospitalini alikuwa hataki kabisa tuzungumzie ugonjwa anaoumwa kwa sababu alijua kwamba umebainika ukiwa katika hatua ya mwisho. Hivyo alijua kwamba ni vigumu kutibika," amesema Mnyika.

Pia ameitaka familia, wanachama na viongozi wa chama hicho kumuenzi kiongozi huyo kwa kutimiza ndoto yake aliyoipambania kwa kipindi kirefu ya kujenga taasisi imara (Chadema), Katiba Mpya, Tume huru ya uchaguzi na kutumia maridhiano kuishinikiza serikali kufikia malengo hayo.

Mwili wa muasisi huyo wa Chadema unatarajiwa kuagwa leo katika Kanisa Katoliki lililoko eneo la Mtaa wa Mwananchi kabla ya kuzikwa katika makaburi ya ya Mtaa wa Mwananchi, Kata ya Mahina jijini Mwanza.

Chanzo: Mwananchi