Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mnyika aitaka Serikali kutangaza tarehe ya mchakato wa katiba

Mnyika 1 Mnyika aitaka Serikali kutangaza tarehe ya mchakato wa katiba

Sat, 9 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amewataka viongozi wa chama hicho mkoani Simiyu kutokaa kimya badala yake wapaze sauti kueleza changamoto zinazowakabili wananchi.

Mnyika ametoa kauli hiyo leo Julai 9, 2022 katika kata ya Lamadi wilayani Busega mkoani Simiyu wakati wa kongamano la chama hicho kuhusu madai ya katiba mpya.

Amesema tangu Juni 22, 2022 Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka alipotoa tamko la CCM kuishauri serikali kufufua mchakato wa katiba mpya, hakuna kiongozi wa serikali aliyejitokeza hadharani kutangaza tarehe ya kuanza kwa mchakato huo.

Pia amewataka wanachama wa Chadema kutobweteka na kauli hiyo ya CCM kuhusu katiba mpya, badala yake amewataka kuongeza juhudi na msukumo ili jambo hilo lifanyike kabla ya uchaguzi wa serikali ya mitaa wa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Toka CCM waseme vile mpaka leo Julai 9, 2022, zaidi ya wiki mbili, hatujasikia kauli ya serikali ikisema imekubali ushauri wa chama kinachoongoza serikali ikisema imekubali na kuufanyia kazi ushauri huo,” amesema Mnyika.

Amesema Chadema kupitia mazungumzo yake na serikali, imeandaa mapendekezo ya mambo ambayo chama kinaona umma unayahitaji kujumuishwa katika Katiba mpya itakayoundwa.

“Mapendekezo ya wananchi yako tayari, kinachosubiriwa ni utekelezaji. Mchakato huu ukifuatwa ni wazi kwamba mchakato wa katiba mpya utakamilika,” amesema Mnyika.

Ameongeza kuwa: “Tukibweteka tukadhani kwa kauli ya CCM tumepata Katiba mpya tutafika 2025 tukiwa hatuna katiba mpya. Tunataka kuhakikisha tunafika mwaka huo tukiwa na katiba mpya.”

Katibu Mkuu huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini, amesema kukamilika kwa katiba mpya ndiyo msingi wa Tume huru ya uchaguzi, hivyo ni muhimu kila chama kihimize kuanza na hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live