Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mnyika afunguka mazito kina Lissu kurejea nchini

Mnyika 1 John Mnyika, Katibu Mkuu CHADEMA

Fri, 10 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya Serikali kutoa hakikisho la usalama wa wanasiasa walioko ughaibuni, akiwamo Tundu Lissu, Godbless Lema na Ezekiah Wenje wa Chadema, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesema taratibu zinafanywa kuhakikisha wanasiasa hao wanarejea.

Lissu, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), aliondoka nchini kwenda kutibiwa Ubelgiji baada ya kupigwa risasi Septemba 7, 2017 na ameendelea kuishi huko kwa hofu ya usalama wake.

Kadhalika, Lema alilazimika kufanya hivyo Novemba 2020 na kuondoka na familia yake, akihofu usalama wake, baada ya kile alichodai kuwa alikuwa akitishiwa maisha.

Hakikisho la usalama na wito wa kurejea kwao lilitolewa bungeni juzi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni aliyesema Rais Samia Suluhu Hassan ametengeneza mazingira mazuri ya kisiasa, hivyo hakuna sababu ya viongozi wa kisiasa, wakiwamo wa Chadema kutorejea nchini.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Grace Tendega, waziri huyo alisema: “Hakuna sababu yoyote kwa Mtanzania aliyeko popote pale, ikiwemo viongozi hao wa Chadema, walioko nje ya nchi kutorejea nchini.

“Ili sio tu waweze kutumia fursa nyingi za maendeleo ya kiuchumi na kisiasa, lakini kushiriki kikamilifu katika kutoa michango yao kwa maendeleo ya nchi yao katika nyanja yoyote kwani hapa ni nyumbani kwao.’’

Jana, Mnyika alisema baada ya kupokea hakikisho hilo la usalama wa viongozi hao, alitoa wito kwao kurejea nchini.

“Sisi kama chama baada ya kauli hiyo ya Serikali tunatoa wito kwa wanachama na viongozi wetu kurejea nchini baada ya kuwa Serikali imetoa kauli ya hakikisho la usalama kwa viongozi wetu wa kitaifa, Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu, wajumbe wa kamati kuu Wenje, Lema na viongozi wengine,” alisema.

Alisema watafanya nao mawasiliano rasmi, ili kujua taratibu nyingine za kurejea kwao.

Lissu bado ahofu

Ingawa kuna hakikisho hilo, lakini Lissu alisema kauli ya Masauni haijibu mahitaji ya kuhakikishiwa usalama wake.

“Nilikimbia kwa sababu ya jaribio la mauaji ambalo halijawahi kuchunguzwa na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria. Ninachohitaji ni kuhakikishiwa usalama wangu. Kauli ya Waziri Masauni haijibu mahitaji hayo,” alijibu Lissu, alipohojiwa na Mwananchi kwa njia ya WhatsApp.

Kinyume na mtazamo wa Lissu, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Lema alisema: “Ni kauli nzuri na nimefurahi kusikia hivyo, kwa sababu hakikisho la usalama sio tu lina faraja kwetu sisi tuliolazimika kukimbia, bali ni kwa watu wengi waliokuwa bado wana hofu”.

Alisema hofu ya mtu mmoja juu ya uhai wake isipuuzwe, huku akisisitiza kuwa amani na haki, ndivyo vitakavyojenga furaha na hatimaye mafanikio.

Ansbert Ngurumo, Mtanzania mwingine aliyekimbilia ughaibuni, alitaka kauli hiyo iambatane na hakikisho la usalama wao, litakalohusisha kuchukuliwa hatua kwa alichodai makumi ya polisi waliohusika katika vikosi vya wasiojulikana.

“Serikali ipige hatua moja mbele, ichukue hatua dhidi ya wahalifu. Hofu haitaisha hadi tuone hatua zinachukuliwa dhidi ya walioshiriki kututisha kwa siri, hadharani na mitandaoni.

“Nitarudi tu, kesho au keshokutwa, lakini kwa sababu nilizokueleza hapo juu, sitarejea kijinga. Kila siku nafuatilia kila hatua zinazochukuliwa za dhati na za kisiasa tu. Naendelea kujipanga na kujiandaa. Wakati utafika, hauko mbali nitapima nitarejea nyumbani, niliondoka kimya kimya lakini sitarejea kimyakimya mtajulishwa,” alisema.

Wasiwasi wa Simbeye

Hoja hiyo iliungwa mkono na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama cha NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye, aliyesema kitendo cha kuwaita nyumbani waliokimbilia nje kuhofia usalama wao bila kushughulikia kikamilifu sababu za msingi zilizowakimbiza, ni kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

“Mfumo wa Serikali uliopo sasa ni ule ule uliokuwepo Lissu aliposhambuliwa kwa risasi. Matukio ya wananchi kufariki wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola bado yanaripotiwa.

“Mfumo wa ulinzi wa usalama na maisha ya wananchi umeparaganyika na kuna haja ya kuangalia utekelezaji wa kanuni na haki ya kuishi kwa mujibu wa Katiba kabla ya kuwaita nyumbani,’’ alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live