Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mlata: Kwa CCM hii, upinzani utaumia

17828 Pic+mlata TanzaniaWeb

Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Monduli. Mpaka sasa wanachama wa Chadema hawamini kilichotokea kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Monduli mkoani Arusha, baada mgombea wao wa ubunge, Yonas Laizer kushindwa na Julius Kalanga wa CCM.

Kalanga alishinda kwa kura 65,714 ikiwa ni asilimia 95 ya kura zote zilizopigwa dhidi ya mpizani wake wa karibu Laizer aliyepata kura 3,187.

Tofauti hiyo kubwa ya kura imewashtua wanachama wa upinzani, lakini Mbunge wa Viti Maalumu CCM Mkoa Singida, Martha Mlata amesema ushindi wao unatokana na umakini wa Serikali ya Awamu ya Tano katika kutekeleza majukumu na ahadi zake.

Akizungumza na Mwananchi digital, Mlata aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, amesema wananchi wamechoshwa na siasa na ahadi zisizotekelezeka zinazofanywa na wameamua kubaki na CCM na wagombea wake.

Mlata ambaye alikuwa miongoni mwa makada wa CCM walioweka kambi kwenye Kata ya Engutoto wilayani Monduli ambako kuna ngome ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amesema sera makini na utendaji kazi wa Serikali vimeimaliza Chadema.

Pia, amewataka wapinzani kutambua kwamba CCM ya sasa si ile ya zamani kwani, wana uongozi imara na uliojikita katika kutatua changamoto za watanzania, hivyo wimbi la ushindi huo litaendelea hadi Uchaguzi Mkuu wa 2020.

“Ingekuwa jambo la kushangaza kama Chadema waliamini wangeshinda, hawana sera wala mipango ya kuwatumikia na kuwapa nafuu ya maisha Watanzania, sasa wanashinda vipi?" amehoji mbunge huyo.

Msimamizi wa Uchaguzi katika jimbo hilo, Steven Ulaya alitaja jana matokeo ya wagombea wengine katika jimbo hilo kuwa ni Elizabeth Michael (AF) kura 16, Wilfred Mlay (ACT Wazalendo – 144), Francis Ringo (ADA-Tadea– 21), Omary Kaigo (DP–34), Simon Ngirisho (Demokrasia Makini – 35) na Feruzy Juma wa NRA kura 45.

Chanzo: mwananchi.co.tz