Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkutano wa nne wa tume ya pamoja kati ya Tanzania na Uganda wamalizika

Odongo.jpeg Picha ya Pamoja Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Balozi Mulamula na Jen. Odongo

Thu, 20 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Uganda wamehitimisha Mkutano wa Nne wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya nchi hizo mbili uliofanyikaa jijini Kampala, Uganda.

Mkutano huo wa siku moja ulitanguliwa na Mkutano Ngazi ya Wataalamu uliofanyika tarehe 17 Januari 2022 na kufuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 18 Januari 2022.

Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huu unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) ambaye ameambatana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.), Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mhandisi Geodfrey Kasekenya(Mb.), Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb.), Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Antony Mavunde (Mb.) na Naibu Waziri Wizara ya Nishati, Mhe. Steven Byabato (Mb.).

Mkutano wa Nne umejadili na kutathimini masuala mbalimbali ya utekelezaji kwenye maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa baina ya nchi hizi. Maeneo hayo ni pamoja na; Siasa na Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Fedha na Uchumi, Nishati, Habari na Mawasiliano, Kilimo, Maendeleo na ujenzi wa Miundombinu, Elimu na Mafunzo, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo na Uvuvi, Maji na Mazingira, Afya na Elimu. Akifungua Mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ameishukuru Jamhuri ya Uganda kwa mapokezi mazuri ya kidugu na uratibu mzuri wa mkutano huo.

Pia, akaeleza imani aliyonayo kwa wajumbe wa mkutano huu ambao walijadili na kutoa maamuzi katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji yaliyowasilishwa kwa ustawi wa mataifa haya, sambamba na kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano kupitia majadiliano hayo.

Pia akafafanua kuwa kupitia ziara za viongozi wetu wakuu Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Yoweri Kaguta Museven, Rais wa Jamhuri ya Uganda changamoto na tozo mbalimbali za kibiashara zilitatuliwa ili kukuza na kuinua urali wa biashara baina ya Tanzania na Uganda.

Kwa upande wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Jen. Jeje Odongo alieleza kuwa Mkutano huu utajadili na kufanya makubaliano katika sekta mbalimbali za ushirikiano zitakazosainiwa katika nyakati tofauti kwa lengo la kufungua maeneo mapya ya ushirikiano ili kuendelea kuimarisha ushirikiano na kutumia fursa zilizopo kwa manufaa ya wananchi wa Nchi hizi mbili.

Aidha, akafananua mkutano huu utajadili hali ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika nchi hizi mbili pamoja na mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaojengwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa pamoja viongozi hao walizitaka sekta zilizopo katika maeneo hayo ya ushirikiano kuhakikisha wanatekeleza na kutatua kwa wakati masuala yote ya kitendaji ili kuruhusu sekta hizo kustawi kiuchumi na kuinua maisha ya Wananchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live