Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Mkimbizi alipoishukuru Tanzania’

2adae532505a0fae1e3bd08e513a8a25 ‘Mkimbizi alipoishukuru Tanzania’

Tue, 15 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

“NINAISHUKURU Serikali ya Tanzania kwamba sikuwahi kupata shida yoyote pale nilipofuata utaratibu hadi kupata ajira hapa Tanzania,” anasema mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kimokrasia ya Congo (DRC), Ebengo John.

Ebengo alitoa ushuhuda huo mwishoni mwa wiki wakati wa warsha iliyohusu masuala ya wakimbizi iliyoandaliwa na tasisi isiyo ya kiserikali ya Dignity Kwanza.

Mkimbizi huyo ambaye ameajiriwa na Shule ya Msingi ya John Bosco kama mwalimu, anasema alipoona tangazo la kazi la shule hiyo na kuomba kisha kukubaliwa, alianza kufuatilia vibali vyote na kupata.

Anasema amekuwa akifanya kazi bila bughudha yoyote huku familia yake ikiwa kambini ambako hukutana nayo kila anapokuwa likizo.

“Wakati ninafuatilia vibali baada ya mwajiri kunikubalia maombi yangu, nilikuwa nina hofu sana, lakini hakuna nilikokwama baada ya kuanza kufuatilia. Nilipata kibali cha kuishi nje ya kambi bila kulipa hata shilingi moja.

“Mbali na kushukuru serikali ya Tanzania, pia ninawaambia wakimbizi wenzangu wachukue ushuhuda kwangu kwamba ukifuata taratibu zilizopo hakuna kokote unapokwama. Tusifuate habari za mitaani. Serikali ya Tanzania ni nzuri sana, naomba iendelee kuwa na moyo huo huo,” anasema.

Ebengo ambaye ana shahada ya uzamili aliyoipata kwao DRC anasimulia kwamba alikimbia nchini humo Novemba 3, mwaka 1996 baada ya kutokea machafuko.

“Siku ya tukio nilikuwa kazini. Nilikuwa mtumishi wa serikali, ndiyo nikaanza kusikia masasi (risasi). Niliponea chupuchupu. Nikakimbia nyumbani kwangu nikakuta familia yangu haipo. Niliikuta njiani wakikimbia na ndipo tukaja Tanzania,” anasema.

Mkurugenzi wa Dignity Kwanza, Janemary Ruhundwa, anasema ingawa Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikibeba mzigo mkubwa wa wakimbizi huku msaada kutoka Jumuiya ya Kintaifa ukiwa mdogo sana, lakini ni wakati wa kufikiria zaidi namna nchi inavyoweza kugeuza changamoto ya wakimbizi kuwa fursa.

“Kama ilivyo kwa Ebengo, wakimbizi wengi ni kama sisi. Wapo wasomi na wenye vipaji mbalimbali lakini kutokana na kukutwa na machafuko na hivyo kuhofia maisha yao wakalazimika kukimbia. La kwanza kabisi hatutakiwi kuwanyanyapaa kwa sababu ni binadanu wenzetu lakini tunaweza kuwageuza kuwa fursa badala ya kuwaona mzigo,” anashauri Janemary.

Katika warsha hiyo, Janemary pia alizungumzia mkakati walio nao wa kuandika kitabu kwa kushirikiana na serikali kitakachoangalia miaka 60 ya Tanzania tangu ilipoanza kupokea na kuhifadhi wakimbizi.

Janemery anasema wakati Umoja wa Afrika unaadhimisha miaka 50 ya kuhifadhi wakimbizi, takwimu zilizopo zinaonesha kwamba Tanzania ilianza kupokea wakimbizi takribani miaka 60 iliyopita.

Lakini Profesa Khoti Kamanga ambaye alikuwa mmoja wa watoa mada katika warsha hiyo anaamini kwamba Tanzania ilianza kupokea wakimbizi baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia.

“Kuna wakimbizi walitoka Holland baada ya vita kuu ya kwanza ya dinia kwa taarifa nilizo nazo. Mkienda pale Tengeru mtapata habari zao kwani kua akaburi yao,” anasema.

Mengi kuhusu mambo yanayotarajiwa kuwemo katika kitabu hicho tutayaona katika gazeti hili Alhamisi ijayo kwenye Jarida la Maarifa.

Chanzo: habarileo.co.tz