Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson, amelazimika kuwatuliza wabunge waliokuwa wanaomba mwongozo wa wake, baada ya sakata la mkataba wa kampuni ya uendeshaji Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kuleta mjadala mpana, huku wabunge wakihoji kutotekelezwa kwa maazimio ya Bunge.
Maazimio hayo ni pamoja na lile la Novemba 2, 2022; ambapo Bunge lilitaka shughuli za uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kuhamishwa kutoka KADCO hadi Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ambalo halijatekezwa hadi sasa licha ya mwaka mmoja kupita.
Ndipo Spika Tulia akataka ufafanuzi: “Mheshimiwa AG naomba unisaidie nani alikuwa anamiliki hicho kiwanja kabla Kadco hawajaja, maana siyo Kadco waliojenga, ama ni Kadico amenga! Nani alikuwa anamiliki hicho kiwanja kabla ya Kadco, Wazir au nani anataka kujibu.”
Ndipo Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akasimama kujibu: “Kiwanja cha Kia kwanza kilikuwa kiwanja cha Serikali, alafu wakati wa ubinafsishaji ikaundwa kampuni ambayo kuna baadhi watu wa sekta binafsi waliingia...baada ya kuona utaratibu ule siyo wa kuridhishwa, Serikali ikaamua kuinunua na wakalipa hiyo hela, na ikatoa maelekezo kuwa kinwanja hicho kilerejwe.”
Mjadala huo umetokea leo Jumamosi, Novemba 4, 2023 ambapo Bunge linajadili taarifa tatu za Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Serikali za Mitaa (LAAC) na ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayoishia Juni 30, 2022.