Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miswada mitatu ya uchaguzi yatua kwa Spika

Tulia 1 660x400 Miswada mitatu ya uchaguzi yatua kwa Spika

Mon, 29 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Mkutano wa 14 wa Bunge la 12 ukianza kesho, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imesema imekamilisha kazi ya kujadili na kuchambua miswada mitatu ya sheria za uchaguzi na kesho itawasilisha taarifa yake wa Spika, Dk Tulia Ackson.

Miswada hiyo ni ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi, na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa, yote ya Mwaka 2023.

Miswada hiyo ilisomwa kwa mara ya kwanza bungeni Novemba 10, 2023 na kupelekwa kwa kamati hiyo kwa ajili ya kujadiliwa na kuchambuliwa.

Kamati ilipokea na kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali kwa siku nne mfululizo kuanzia Januari 6 hadi 10 mwaka 2024. Ilipokea maoni kutoka kwa watu na taasisi 1,707.

Baadhi ya maoni yaliyowasilishwa kwenye kamati hiyo ni kutaka wakurugenzi wa halmashauri wasisimamie uchaguzi na kiwepo kifungu kinachotoa takwa la ushindi wa kura za urais kuwa zaidi ya asilimia 50, matokeo hayo kupingwa mahakamani na vyama vya siasa vyote kupewa ruzuku.

Maoni mengine ni kuondolewa kwa gharama za kuchukua fomu, vyama kulazimishwa kuteua asilimia 50 ya wagombea wanawake katika uchaguzi, ili kufikia usawa wa kijinsia katika uongozi na kurekebishwa kwa kifungu kinachoeleza uteketezaji wa nyaraka za uchaguzi baada ya miezi sita.

Hata hivyo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ni miongoni mwa vyama 13 vya siasa vilivyowasilisha maoni mbele ya kamati hiyo, kilipendekeza kufutwa na kuondolewa bungeni kwa miswada hiyo ya sheria na badala yake muswada wa marekabisho ya Katiba upelekekwe bungeni kuweka msingi wa mabadiliko husika.

Januari 13, 2024, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alitangaza maandamano Januari 24, 2024 yaliyolenga kushinikiza kuondolewa bungeni kwa miswada hiyo mitatu ya uchaguzi pamoja na ugumu wa maisha.

Maandamano hayo yalifanyika Januari 24, mwaka huu na ujumbe wake ulipokewa kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) zilizopo jijini Dar es Salaam.

Licha ya hali hiyo, leo Januari 28, 2024 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Joseph Mhagama amesema kamati imekamilisha majadiliano na uchambuzi wa miswada hiyo tayari kwa hatua inayofuata.

“Tumeshakamilisha majadiliano na uchambuzi, kesho namuandikia Spika kuhusu kukamilika kwa majadiliano na uchambuzi,” amesema Dk Mhagama alipoulizwa na Mwananchi Digital.

Amesema baada ya hapo atawasilisha taarifa ya kukamilika kwa majadiliano na uchambuzi wa miswada hiyo kwa Kamati ya Uongozi ya Bunge (inayoongozwa na Spika) kwa ajili ya uamuzi.

Amesema baada ya leo, ndiyo itafahamika iwapo miswada hiyo itaenda bungeni katika mkutano wa Bunge wa 14 unaoanza Jumanne au la, kama kanuni za Kudumu za Bunge zinavyoelekeza kuhusu utaratibu wa utungaji wa sheria.

Hoja nyingine kuibuka

Wakati miswada hiyo ikitarajiwa kuamuliwa na Kamati ya Uongozi, suala la kupanda kwa bei ya sukari nchini hadi kufikia au kuzidi Sh5,000 kwa kilo linaelezwa linaweza kuwa moja ya mijadala moto kwenye mkutano huo.

Vilevile kuchelewa kukamilishwa miradi ya maendeleo, ikiwemo iliyoibuliwa na kuchangiwa na wananchi linatajwa litajitokeza.

Mbali ya hayo, kuharibika miundombinu ya barabara kutokana na mvua kuongeza bei ya mazao kutokana na kupanda kwa gharama usafirishaji, nalo linaelezwa huenda likawa sehemu ya hoja bungeni.

Mbunge wa Manyoni Mashariki, Dk Pius Chaya amesema mwaka huu ni wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na wananchi wana imani kubwa ya kukamilika kwa miradi iliyopangwa.

Amesema kwa kuwa Serikali katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 Desemba mwaka jana ilitangaza kukusanya Sh13 trilioni, basi uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo upo kwa sababu fedha zipo.

Alisema iwapo Muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma wa mwaka 2023, utaingia bungeni katika mkutano wa 14 wa Bunge, utakuwa msaada mkubwa kwa Serikali kwa sababu utaboresha utendaji wa mashirika ya umma.

“(Four R), R nne ndiyo ndoto ya Rais Samia Suluhu Hassan nina imani maoni ya wananchi yakifanyiwa kazi yatasaidia sana Serikali ya awamu ya sita,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema hoja za kupanda kwa bei ya sukari inagusa masilahi ya watu wengi, hivyo ni vyema Serikali ikajifunza kutoka kwenye mazao mengine kama mbegu za mafuta.

“Ni hoja yenye nguvu na masilahi kwa wananchi, hivyo ni vyema ikajadiliwa bungeni, ili kupatiwa ufumbuzi wa kina,” amesema.

Mkazi wa Nkuhungu jijini Dodoma, Diana Laswai amesema kuharibika kwa miundombinu ni hoja ya kiuchumi ambayo inatakiwa kujadiliwa kwa kina bungeni.

Amesema Serikali ielekezwe kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hiyo.

“Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, mafuriko, uharibifu wa miundombinu ni vitu tunavyovitegemea, ni vyema Serikali ikatenga bajeti ya kutosha ya dharura kila mwaka,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live