Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Millya awananga wanaokimbilia CCM

10586 Pic+milya TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mirerani. Mbunge wa Simanjiro (Chadema), James ole Millya amesema hakuhamia chama hicho kikuu cha upinzani nchini kwa kufuata mtu, bali alifuata haki.

Millya ambaye alijiunga Chadema akitokea CCM na kupitishwa kuwania ubunge na kuibuka ushindi, alisema anampenda Rais John Magufuli kwa kuwa pia ni mpenda haki.

Alitoa kauli hiyo juzi katika mji mdogo wa Mirerani mbele ya Waziri wa Madini, Angellah Kairuki kwenye kikao cha kujadili utaratibu wa uchimbaji madini na Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (Marema).

Alisema kwa kupenda haki aliamua kujitoa CCM na kujiunga na Chadema mwaka 2012 akiwa na kero zaidi ya 20,000 baada ya kuona hakuna haki wala demokrasia.

Millya alisema watu wengi wanatambua historia yake na kuwataka wananchi walioshiriki kikao hicho kuacha kujidanganya kwa kushangilia ‘CCM oyeee’ wakati kwa namna moja au nyingine walishiriki kutorosha madini bila kulipa kodi ya Serikali.

Kumekuwa na wimbi la wabunge na madiwani kutoka upinzani kuhamia CCM wakieleza ni kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli.

Hatua hiyo pia imesababisha kufanyika kwa chaguzi nyingi za marudio.

“Rais Magufuli hana chama kwenye suala la wizi kwani hata wanaCCM ambao ni wezi amewakamata, hivyo baadhi yenu msijidanganye kwa kusema CCM oyeee kinachopaswa kuangaliwa na kutangulizwa mbele ni maslahi ya Taifa,” alisema Millya.

Alipongeza hatua ya ujenzi wa ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite uliofanywa na Rais Magufuli, kwani kwa vyovyote utachangia kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo huku watu watakaofanikiwa kupata watalipa kodi na mrabaha kwa Serikali.

“Tushirikiane na mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ili kufanikisha maendeleo bila kuingiza siasa au kupotosha lengo la ukuta uliowekwa na Rais Magufuli mimi naunga mkono ukuta huo utatusaidia kuona faida ya madini ya Tanzanite,” alisema Millya.

Naye rais wa shirikisho la vyama vya wachimbaji madini nchini, John Bina alisema viongozi wa wachimbaji wa Tanzanite wanapaswa kuachana na harakati zisizo na mashiko badala yake washirikiane vyema na Serikali.

“Pamoja na hayo tunapaswa kutambua kuwa kuchimba Tanzanite ni tofauti na dhahabu kwani unaweza kufanya kazi kwa zaidi ya miaka mitano usipate kitu, hivyo Serikali na wachimbaji wadogo wanapaswa kuona hilo,” alisema.

Awali, akizungumza kwenye kikao hicho, katibu wa Marema tawi la Mirerani, Abubakary Madiwa alisema wamiliki na wachimbaji wamewekeana mikataba ya kugawana uzalishaji unapofanyika.

Naye kaimu mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Tumaini Magessa alisema kwamba Waziri Kairuki atarejea tena mji mdogo wa Mirerani Agosti 9 ili kutoa uamuzi wa majadiliano hayo.

Chanzo: mwananchi.co.tz