Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imemuengua Mgombea wa nafasi ya Uwakilishi Jimbo la Mtambwe, Mkoa - Kaskazini Pemba, Mohammed Ali Suleiman (ACT WAZALENDO), kwa kile kinachodaiwa udanganyifu wa Kitambukisho la Mzanzibar Mkaazi.
ZEC Kisiwani Pemba imethibitisha hilo na kusema kuwa Mgombea huyo aliwekewa pingamizi Kwa Madai ya kuwa na vitambulisho viwili vya Mzanzibari Mkaazi vinavyosomeka kwa namba mbili tofauti jambo ambalo ni kosa kisheria.
Mgombea Ali Suleiman anadaiwa kufanya udanganyifu wa kutoandika namba sahihi inayopaswa kutumika katika fomu yake na kufanya Mgombea huyo kupoteza sifa.
Katibu wa Idara ya Habari na Uenezi wa Chama cha ACT-Wazalendo Salum Biman amesema hadi sasa hawajapata taarifa rasmi za kuenguliwa Mgombea huyo licha ya kuona Taarifa hizo kwenye mitandao ya Kijamii.
"Tumezisikia taarifa ila bado hatujapokea Taarifa rasmi kutoka ZEC juu ya kuenguliwa kugombea Uwakilishi kwa Mgombea wetu katika jimbo la Mtabwe Pemba," Amesema Bimani.
Jimbo la Mtambwe linafanya Uchaguzi mdogo Baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo Habib Mohammed Ali wa ACT WAZALENDO kufariki Dunia mwanzoni kwa mwaka huu.