Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgombea urais wa Ada Tadea aahidi kampeni za kistaarabu

7476377508f2e6f038533418842ae2e9 Mgombea urais wa Ada Tadea aahidi kampeni za kistaarabu

Thu, 30 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha Ada Tadea, Juma Ali Khatib, amesema chama chake kimejipanga kufanya kampeni za kistaarabu zitakazozingatia maadili na kanuni za uchaguzi kwa ajili ya kujenga mshikamano na kudumisha amani na utulivu nchini.

Khatib alisema hayo baada ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Dar es Salaam juzi kumchagua kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, kwa kupata kura 126 kati ya 130 zilizopigwa.

Akizungumza na HabariLEO jana mara baada ya kuwasili Zanzibar katika ofisi ya chama hicho, Khatib alisema chama chake kimejipanga kufanya kampeni za kistaarabu kwa mujibu wa makubaliano ya kanuni za uchaguzi mkuu.

“Chama change kinatambua kuwa mara baada ya harakati za kampeni kumalizika maisha yataendelea kama kawaida, kwa hivyo hakuna sababu ya kusababisha malumbano, mifarakano na uhasama unaoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa taifa.”

''Chama chetu kimetia saini makubaliano ya kutekeleza na kusimamia kanuni za uchaguzi yaliyoratibiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), hivyo tunaahidi kufanya kampeni zitakazojenga umoja na mshikamano bila ya kutukanana katika majukwa,” alisema.

Mgombea huyo wa urais kupitia Ada Tadea alitaja mambo ya msingi ambayo yanakusudiwa kutekelezwa na chama hicho endapo kitachaguliwa kuingia madarakani, ni kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayosimamiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwa ajili ya kuimaliza kwa manufaa ya wananchi.

Alisema miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa bandari kubwa ya kisasa ya Mpigaduri iliyopo Maruhumbi mjini Unguja na bandari ya kuhifadhi mafuta ambayo ujenzi wake unaendelea Mangapwani mkoa wa Kaskazini Unguja.

Aidha, alisema wajawazito mara watakapojifungua watapewa fedha za kujikimu kwa ajili ya matunzo ya watoto wao ili waweze kupata makuzi bora na kuwa na afya njema.

''Hiyo ndiyo mikakati yetu ya utekelezaji wa Ilani yetu ya uchaguzi, pia tutatekeleza na kumaliza miradi ambayo itaachwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein,” alisema.

Wanachama na wafuasi wa Ada Tadea walifurika katika ofisi ya chama hicho zilizopo Mwanakwerekwe kwa ajili ya kumpokea mgombea huyo wa urais baada ya kuchaguliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Katibu Mwenenzi wa Ada Tadea, Rashid Mshenga, alisema wamefurahishwa na ushindi mkubwa alioupata mgombea wao, akieleza kuwa ni ishara kwamba anakubalika katika chama na wanachama.

''Chama cha Ada Tadea sasa kipo tayari kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba kwa nafasi ya urais baada ya kupata mgombea atakayepeperusha bendera ya chama chetu,'' alisema.

Uchaguzi huo wa Ada Tadea pia umemchagua John Shibuda kuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano baada ya kupata kura 120.

Chanzo: habarileo.co.tz