Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgombea urais Ada Tadea kuondoa kodi za vyakula

5061068d06dbab171da494b9d08533e8 Mgombea urais Ada Tadea kuondoa kodi za vyakula

Fri, 16 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Ada Tadea, Juma Ali Khatib amesema akichaguliwa kuwa rais anakusudia kuondoa kodi katika bidhaa muhimu za vyakula ili kuleta unafuu kwa wananchi katika kufanya manunuzi.

Khatib alisema hayo akiwa Gando Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati alipohutubia mkutano wa hadhara wa kampeni ambapo alisema bei ya bidhaa nyingi muhimu za chakula wakati zinapofika Pemba bei yake huongezeka.

Alivitaja vyakula ambavyo atapunguza ushuru ili kutoa unafuu kwa wananchi ni mchele, unga wa ngano, sukari pamoja na mafuta ya kula.

“Nikichaguliwa kuwa rais nakusudia kupunguza kodi ya ushuru kwa bidhaa za vyakula zinazoingia katika kisiwa cha Pemba, mara nyingi vyakula vinapoingia Pemba kutoka Unguja bei yake huongezeka kutokana na ushuru na usafiri hadi kuvifikisha kijijini kwa wananchi,”alisema.

Alisema chama chake kitaendeleza dhamira yake ya ujenzi wa bandari ya Wete ili iweze kuwaunganisha wananchi wa kisiwa hicho na mikoa jirani ikiwemo Mombasa, Kenya.

Alisema kuwepo kwa bandari hiyo kwa kiasi kikubwa itasaidia kukuza na kuimarisha huduma za usafiri kwa wananchi, hatua ambayo itasaidia kuleta maendeleo ya ukuaji mkubwa wa kiuchumi.

‘’Chama changu kikifanikiwa kuingia Ikulu bado kina dhamira ya dhati ya ujenzi wa bandari ya kisasa Wete Pemba ambayo itasaidia ukuaji wa kiuchumi kwa wananchi wa kisiwa hicho na kufanya biashara na nchi jirani,” alisema.

Naye Katibu Mwenezi wa Chama cha Ada Tadea, Nuru Kimwaga alisema chama chake kimejipanga kuleta mabadiliko makubwa ya maisha ya wananchi wa Unguja na Pemba na kuwataka kukipa ridhaa ya kuongoza.

‘’Wananchi wa Pemba tupeni ridhaa ya kuongoza nchi, tumejipanga vizuri kuleta mabadiliko makubwa ya maisha ya wananchi kuwa bora kwa kutumia ilani yetu,”alisema.

Jumla ya wanachama wapya 100 wamejiunga na chama hicho baada ya kuvihama vyama vya ACT-Wazalendo pamoja na CUF.

Chanzo: habarileo.co.tz