Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgombea udiwani SAU avunja rekodi kwa vituko

11966 Pic+sau TanzaniaWeb

Wed, 15 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mgombea udiwani katika Kata ya Mawenzi kwa tiketi ya Sauti ya Umma (SAU), Issack Kireti ambaye ameambulia kura mbili, anaweza kuwa mgombea aliyevunja rekodi kwa vituko na ahadi za kufikirisha.

Anapoingia kwenye mkutano wa kampeni akitumia usafiri wa pikipiki ya kukodi maarufu kama bodaboda, unaweza kudhani ndio mpiga debe aliyekuja kuandaa mkutano, lakini baadaye unagundua kuwa ndiye mgombea.

Hushuka kwenye pikipiki na kumruhusu dereva kuondoka, kisha hutoa kipaza sauti chake na kuanza kujitambulisha kabla ya kuanza kumwaga sera ambazo huwaacha hoi watu.

Mawakala wamwangusha

Safari hii alipogombea tena nafasi ya udiwani, Kireti aliamini angeshinda kwa asilimia kama 70, lakini anasema mawakala wa Chadema na CCM aliowaamini wamwangalizie kura zake ndio wamemuangusha.

Mgombea huyo aliyeonekana kama mchekeshaji katika kampeni zake, anadai kuwa katika vituo vya kupigia kura, hakuwa na wakala yeyote wa SAU bali aliwaamini mawakala wa Chadema na CCM kuwa wangemlindia kura.

“Mimi sikuwa na mawakala ila kuna watu tu walijitokeza wakasema watanisaidia kusimamia kura zangu. Wengine walikuwa ni wa Chadema na wengine wa CCM ila sikuwaamini sana,” alidai.

Mgombea huyo alidai anaamini kama angekuwa na mawakala huenda matokeo hayo yasingekuwa hivyo, kwani katika watu ambao walikuwa wanapendwa na wapiga kura ni yeye.

Mgombea mzoefu

Katika uchaguzi huo uliofanyika Agosti 12, 2018, Kireti aliambulia kura mbili ikiwamo ya kwake, huku mgombea wa CCM, Apaikunda Naburi akishinda kwa kura 400, na Afrikana Mlay wa Chadema akipata kura 163.

Novemba mwaka jana, Kireti aligombea udiwani katika Kata ya Bomambuzi mjini Moshi na kuambulia patupu huku Juma Raibu wa CCM akiibuka mshindi kwa kupata kura 2,854.

Si tu udiwani, katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Kireti aligombea ubunge wa Moshi mjini na kushika nafasi ya nne kwa kupata kura 181 huku Jaffar Michael wa Chadema akishinda kwa kupata kura 51,646.

Alivyopokea kura mbili

Akizungumza na gazeti hili, Kireti anadai ameyapokea matokeo hayo kwa mshangao kwa vile alikuwa anaungwa mkono na wananchi wengi wa kata ya Mawenzi kutokana na sera zake.

“Nimeyaona haya matokeo kwa kweli yamenishangaza sana. Katika watu waliotoa sera nzuri ni mimi. Kuna mtu aliahidi kujenga gereza la ghorofa kwa ajili ya mafisadi kama mimi?” anahoji Kireti.

“Hili gereza nilisema nitaweka swimming pool (bwawa la kuogelea) na TV. Nikasema nitajenga Flyovers (barabara za juu), kutenga maeneo ya machinga na kupanda miti mbalimbali ya matunda.

“Kikubwa nilichotamani kukifanya katika hili gereza la ghorofa ni kutenga vyumba ambavyo tutawapelekea hao mafisadi wake zao ili wakate kiu. Hii itaendeleza ndoa zao na kuzuia watoto wasizaliwe nje ya ndoa.

“Niliahidi pia kukomesha wizi wa kanyaboya, rushwa na kupambana na kukosekana kwa taa za barabarani. Lakini naona wameamua kunitosa, kwa hiyo rushwa itaendelea kuwatafuna,” anaeleza.

Kireti anaongeza sababu nyingine ya kushindwa uchaguzi huo akidai alichokigundua katika uchaguzi huo, mashabiki wake wengi hawakuwa wamejiandikisha kupiga kura katika kata hiyo.

Awatosa viongozi SAU

Akizungumzia sababu ya viongozi wa chama hicho kutoshiriki katika kampeni zake, Kireti alidai kuwa aliamua kuwatosa baada ya kutomtumia fedha za kampeni kama walivyokuwa wameahidi.

“Chama changu hakikuwa na ruzuku wala mfadhili. Hizi kampeni nimeziendesha mwenyewe. Nilifanya mikutano mikubwa sita na midogo minne. Si haba kwa hali ilivyokuwa,” anasema.

Katika mikutano yake ya kampeni, Kireti alikuwa akienda peke yake wakati wote na wakati mwingine wapita njia ndio walikuwa wakimnyanyua mikono kwa kupokezana wakati wa kumnadi kwa wapiga kura.

Ahadi zake za 2015

Wakati akigombea ubunge Jimbo la Moshi, Kireti aliendeleza ahadi zake alizozianza 2015 na wakati huo akaahidi kupigania kima cha chini ya mshahara kiwe Sh1 milioni kwa mwezi.

Kireti pia akaahidi pia atahakikisha wakazi wa jimbo lake wanapata mlo mzuri kuanzia asubuhi na kusisitiza kuwa ni lazima kila mpiga kura awe anakula kuku mzima badala ya kipande.

“Nataka kila mtu asubuhi akiamka anapata breakfast (kifungua kinywa) chenye mapochopocho yote kuanzia mayai, kachumbari, matunda na supu,” anasema Kireti na kuongeza;

“Mwaka 2010 nilipokuwa nagombea ubunge niliahidi mshahara wa Sh600,000 si mliona Serikali ikapandisha mishahara hadi 120,000? Leo nimekuja na Sh1 milioni.”

Katika ahadi nyingine iliyowaacha hoi wananchi wa jimbo hilo wakati huo ni ya kujenga gereza la kisasa la ghorofa katika eneo lilipo gereza la sasa la Karanga ili lifanane na magereza ya nchi za Ulaya.

“Kuna mahabusu wa mauaji wanakaa miaka minane hadi 10 gerezani, lakini mwisho wa siku anaachiwa. Kwanini huyo aishi kwa mateso? Nitajenga gereza la ghorofa,” anasema Kireti.

Hata hivyo, pamoja na ahadi zake hizo na zile za kupanda miti ya matunda jimbo zima ili wananchi wake wasinunue matunda, hakuweza kufurukuta dhidi ya mbunge wa sasa, Jaffar Michael.

Alikuwa akiwaacha hoi zaidi mashabiki wake, pale alipowaahidi katika mikutano yake hiyo kuwa kama angeshinda ubunge, angekwenda kuapishwa bungeni na viatu aina ya makobazi.

“Nitakuwa wa mwisho kununua viatu vipya. Hivi mnavyoviona (akionyesha makobazi aliyovaa) ndio nitaenda navyo bungeni na nitarudi navyo kuja hapa kuwashukuru.

“Nawaambia sitakaa nibadili viatu hivi nilivyochapa navyo lapa wakati wa kampeni. Sipiganii madaraka kwa ajili ya kujinufaisha. Mtaniona navyo hivi hivi,” anasisitiza.

Kireti ambaye hotuba zake zimekuwa zikiwavunja mbavu wasikilizaji, alitoa mpya pale aliposema yeye atakuwa mbunge wa mwisho nchini kununua gari la kifahari kama wenzake.

“Hivi vyama vikubwa vinapenda magari ya kifahari. Hawana tofauti na chawa na viroboto. Si mnajua kazi ya chawa na viroboto ni kunyonya damu? Sitaki kunyonya damu yenu,” anasema.

Ahadi zake za 2010 zilitia fora

Katika uchaguzi mkuu wa 2010, Kireti alijitosa kwa mara ya kwanza na alitoa mpya pale alipowaeleza wananchi kuwa, kama atachaguliwa atahakikisha wanakula nyama na samaki kila siku ili wanenepe.

Alienda mbali na kuahidi kuwa kima cha chini cha mshahara kinakuwa Sh600,000 kwa mwezi na kuhalalisha ulaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi kama ilivyo nchini jirani ya Kenya.

Kuna wakati Kireti alilazimika kuhamishia mikutano yake katika vijiwe vya kahawa ili kuwafuata wananchi baada ya eneo la awali alilokuwa amepanga kufanyia mkutano kutokuwa na watu.

“Watanzania wanakondeana kwa sababu ya njaa wanahitaji kula nyama na samaki ili waliokonda wanenepe na wale wenye mvi wakati ni vijana warudie kwenye ujana wao. Nataka wajaziane kama wenzao wa Kenya,” anasema.

Muda wote wakati mgombea huyo akihutubia, wananchi wachache wanaohudhuria au wapita njia walikuwa wakivunjika mbavu kwa vicheko.

Chanzo: mwananchi.co.tz