Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgombea ubunge DP Monduli asema kipaumbele chake ni elimu

Wed, 5 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Monduli. Mgombea ubunge (DP) Monduli jijini Arusha, Omar Kawaga amesema kipaumbele chake cha kwanza akichaguliwa ni kuhakikisha watoto wote wa jamii ya kifugaji wanakwenda shule.

Akizungumza na Mwananchi, Kawaga ambaye anaendelea na kampeni za mtu kwa mtu na nyumba kwa  nyumba, akisubiri viongozi wa kitaifa wa chama hicho kuja Monduli kuzindua kampeni zake, alisema anawaomba wananchi Monduli wamchague ili atimize ahadi hiyo.

"Mimi kipaumbele changu cha kwanza ni elimu kwani bila elimu kwa vijana wetu hatuwezi kupata maendeleo, nikichaguliwa nataka kukaa na wazee wa jamii ya kifugaji tuwe na mikakati ya pamoja kuhakikisha watoto wanasoma," alisema.

Alisema jambo jingine kubwa ambalo atalishughulikia ni suala la migogoro ya ardhi kwani, imekuwa kero kubwa katika wilaya hiyo, kutokana na watu wachache kumiliki ardhi na kushindwa kuiendeleza.

Akizungumzia hali ya kampeni, alisema inakwenda vizuri lakini wanasiasa wanapaswa kuvumiliana na vijembe vya kampeni kwani ndio siasa.

"Nimesikia CCM na Chadema wakituhumiana hizi ndio kampeni lazima tuwe wavumilivu na tuendelee kutafuta kura," alisema.

Alisema hadi sasa ana imani na wasimamizi wa uchaguzi kwani hakuna dosari ambayo imejitokeza na hivyo akawataka wananchi wa Monduli kumchagua yeye awe mbunge wao.

Chanzo: mwananchi.co.tz