Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgombea ubunge Chadema asema maisha yanaendelea

17816 Pic+asia TanzaniaWeb

Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa mgombea ubunge wa Ukonga kwa tiketi ya Chadema, Asia Msangi amesema hajashtushwa na matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo kwa kuwa dalili zilianza kuonekana mapema jana asubuhi.

Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 17, 2018 Msangi amesema kitendo cha mawakala kuzuiwa kuingia vituoni na mazingira yaliyozunguka uchaguzi huo yalihalalisha  ukandamizwaji wa demokrasia.

Amesema dalili za kuangushwa kwake zilianza kuonekana saa mbili asubuhi kutokana na mchezo mchafu uliofanywa ili asishinde.

“Maisha yanaendelea, nawashukuru sana wakazi wa Ukonga wameonyesha kunikubali mno ila mazingira yaliyopo ni kama walivyojionea. Niwape pole kwa yote yaliyotokea tuache kila jambo lina mwisho wake,” amesema.

“Nawasihi wasife moyo tutafanya kazi kwa kuwa yale yote niliyokuwa nikiwaambia yapo kwenye fremu ya kichwa changu tutashirikiana kuyafanyia kazi kwa kuwa na mimi ni mkazi wa Ukonga,”

Kuhusu hatua zipi zitafuata Msangi amesema, “Bado nipo na wanasheria wangu na viongozi wangu wa chama tunaendelea kujadiliana, tukifikia uamuzi tutawataarifu kwa sasa ni mapema mno kutoa msimamo wa chama.”

Katika uchaguzi uliofanyika jana Septemba 16, Tume ya uchaguzi ilimtangaza mgombea wa CCM, Mwita Waitara kuibuka mshindi na kuendelea kulitumikia jimbo hilo.

Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo la Ukonga Jumanne Shauri alimtangaza Waitara kuwa mshindi kwa kura 77,795  sawa na asilimia 89.19 na Msangi alipata kura 8676 sawa na asilimia 9.95.

Watu waliotarajiwa kupiga kura ni 300,609 ila waliojitokeza ni 88270 sawa na asilimia 29.4

Chanzo: mwananchi.co.tz