MGOMBEA ubunge katika Jimbo la Monduli kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fredrick Lowassa, amemwomba mgombea urais wa chama hicho, John Magufuli kumpatia maji katika jimbo pindi atakapochaguliwa kuwa rais.
Aliomba maji lita milioni 100 ambayo ni ziada ya maji yatakayokuwa yanapatikana katika Mkoa wa Arusha pindi mradi Sh bilioni 520 utakapokamilika, yaelekezwe katika jimbo lake kutatua kero ya maji.
Lowassa alitoa ombi hilo jana katika Uwanja wa Shehe Amri Abed mkoani Arusha alipopata nafasi ya kuomba kura na kusalimia wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni wa mgombea urais huyo kupitia CCM ambaye kwa sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Awali, Magufuli alitaka mkandarasi na viongozi watakaokuwa wamechaguliwa, kushirikiana na mbunge ili ifikapo Desemba, 2020 wananchi wa Arusha waanze kutumia maji.
Magufuli alimtaka mkandarasi afanye kazi usiku na mchana ili Desemba akabidhi mradi.