MGOMBEA ubunge katika Jimbo la Nanyamba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Chikota, ameipongeza serikali kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho katika jimbo hilo na Mkoa wa Mtwara kwa jumla.
Alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za CCM katika Kata ya Mtiniko jimboni humo.
Alisema katika miaka mitano ya uongozi wa Awamu ya Tano, serikali imefanya mambo mengi mazuri katika halmashauri hiyo hususan katika sekta zinazogusa huduma za jamii, ikiwemo ya ujenzi wa hospitali ya wilaya iliyogharimu zaidi ya Sh bilioni 1.
Aidha, Sh bilioni 1.4 zimetumika kwa ujenzi wa vituo vitatu vya afya katika maeneo ya Majengo, Dinyecha na Kilomba katika halmashauri hiyo. Chikota alisema ujenzi wa zahanati 11 unaendelea na pia, halmashauri imepata magari matatu likiwemo la mganga mkuu na la wagojwa.
Alisema wananchi wameanza kunufaika na ujenzi wa Barabara ya Mtwara -Mnivata kwa kiwango cha lami unaoendelea na barabara za mzunguko za ndani ya halmashauri na kila mwaka zinajengwa kilometa 2 kwa kiwango cha lami.
Chikota alisema huduma za maji safi na salama zimeongezeka kutoka asilimia 41 hadi 47, lakini pia Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) inajenga minara 11 ya simu katika halmashauri hiyo.
Katika mkutano huo, mgombea ubunge Jimbo la Newala Mjini, Kapteni mstaafu George Mkuchika aliomba wananchi wawachague wagombea wa CCM.
"Tupige kura nyingi kwa CCM kwani uchaguzi uliopita CCM tulipoteza majimbo matatu ya uchaguzi ikiwemo Mtwara Mjini, Ndanda na Tandahimba pamoja na kata 62 kwa hiyo msichague mtu ambaye hana serikali; chagueni mtu mwenye serikali," alisema Mkuchika.
Mgombea ubunge Jimbo la Tandahimba, Ahmad Katani alisema wakati akimnadi Chikota kuwa, wananchi mkoani humo hawana budi kuwachagua wagombea wa CCM ili serikali iendelee kuwale