Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgombea: Chagueni mtu badala ya chama

B3b90f3212d0f68b76ba57b73bbd891e Mgombea: Chagueni mtu badala ya chama

Mon, 14 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA ubunge jimbo la Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) Kiza Mayeye ametoa wito kwa wapiga kura kuangalia mgombea mwenye dhamira ya kuwaleta maendeleo badala ya kuchagua mgombea kwa kufuata vyama.

Aliyasema hayo wakati akizundua kampeni za ubunge na udiwani katika jimbo hilo lililopo katika wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma.

Alisema mgombea mwenye dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi anaweza kutoka chama chochote cha siasa.

Ameunga mkono jitihada za Rais John Magufuli kuwaletea wananchi maendeleo bila kuangalia kama eneo anatoka mgombea wa upinzani au CCM lakini miradi mikubwa imefanyika na kwamba hata katika maeneo ya wabunge na madiwani wa CCM zipo changamoto nyingi za kimaendeleo kushinda kwenye majimbo ya wapinzani.

“Rais Magufuli amefanya kazi kubwa ya kupeleka miradi kwa wananchi bila kubagua kwamba huyo ni mpinzani na hiyo inatokana na dhamira ya kweli ya kuwatumia wananchi, nipeni nafasi ya kuwa Mbunge nikafanye kazi naye ili kuhakikisha namsimamia kwa karibu ili miradi mingi ya maendeleo iweze kutekelezwa kwenye jimbo letu ,msiangalie chama angalieni mtu atakayesimamia maendeleo yenu”alisema mgombea huyo.

Alisema upatikanaji wa maji safi na salama bado changamoto kubwa kwenye jimbo hivyo atakapochaguliwa kuwa Mbunge atasimamia kwa karibu kuhakikisha miradi mingi ya maji inatekelezwa na maji yanafika karibu na maeneo wanayoishi wananchi.

Mayeye alisema ajira kwa vijana bado ni tatizo kwa wananchi wa jimbo na kwamba miradi ya kilimo inatoa ajira kubwa kwa vijana ikiwekewa miundo mbinu wezeshi ya kukifanya kuwa na tija kwa kuwekewa mazingira ya uzalishaji wenye tija sambamba na kutafutwa kwa masoko ya bidha hizo za kilimo.

Awali Diwani wa kata ya Mahembe, Mamisho Seifu akizungumza katika mkutano huo aliwaomba wapiga kura wasipumbazwe na historia za baadhi ya wagombea waliosoma au kuishi Ulaya kwani dhamira ya kweli ya kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi inatoka mioyoni mwa wagombea na siyo kutoka Ulaya.

Diwani wa kata ya Kidahwe katika jimbo la Kigoma Kaskazini, Mchungaji Justin Lukele alisema wagombea wa chama hicho kwa ngazi ya urais, ubunge na udiwani wamejipanga kuhakikisha wanaleta maendeleo ya kweli kwa wananchi na hivyo wananchi wawachague wagombea wa CUF.

Chanzo: habarileo.co.tz