Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgombea Chadema aahidi kuvalia njuga kero ya maji

10214 CHDEMA+PIC TanzaniaWeb

Sun, 5 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Mgombea ubunge wa Chadema katika Jimbo la Buyungu, Kigoma, Eliya Kanjero ameahidi kutatua kero ya ukosefu wa maji ya bomba katika vijiji vingi vya jimbo hilo endapo atashinda katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo.

Akizungumza na wakazi wa vijiji vya Churazo na Nyamuirunde Kata ya Nyamtukuza, Kanjero alisema tatizo la maji ni kubwa na halina budi kuwekewa mikakati maalumu ili kulitatua.

“Nimejaribu kulisemea nikiwa diwani katika vikao vyetu vya madiwani lakini serikali imekuwa ikitoa ahadi zisizotekelezwa, sasa nawaomba mnichague niwe mbunge wenu ili niwabane halmashauri pamoja na serikali kuu kwa uhakika zaidi,” alisema Kanjero.

Tatizo la maji ambalo ni sugu jimboni humo limekuwa likisemewa mno na wagombea ubunge, lakini miradi mingi ya maji inayoanzishwa inadaiwa kufujwa.

“Nipeni ubunge nikawashughulikie viongozi na watendaji wanaohujumu miradi yetu na kusababisha mama zetu kuteseka, nina uhakika ndani ya miaka miwili hii mtaona mabadiliko kwa sababu nitaanzia alipoishia marehemu Kasuku Bilago,” alisema.

Katibu wa Chadema mkoa wa Kigoma, Shaban Madede alisema wakazi wa Buyungu hawana budi kumchagua mgombea wa chama hicho ili wapate mabadiliko kwani jimbo hilo lipo nyuma kimaendeleo.

Hili jimbo limeongozwa na wabunge wa CCM kwa miaka mingi lakini hawakuleta maendeleo yoyote ya kujivunia, lakini miaka miwili na nusu chini ya marehemu Bilago (Chadema) sasa kuna mabadiliko na maendeleo yanaanza kuonekana,” alisema Madede.

Chanzo: mwananchi.co.tz