Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgombea CCM jimbo la Lissu arejesha fomu, 12 bado

67360 Lissu+pic

Thu, 18 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Singida. Wakati leo Alhamisi Julai 18, 2019 saa 10 jioni ndio siku ya mwisho ya uchukuaji na urejeshaji fomu za kuomba kuteuliwa kugombea ubunge Singida Mashariki, mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Miraji Mtaturu ndiye pekee aliyerejesha fomu.

Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Ikungi, Thomas Mwailafu akizungumza na Mwananchi amesema hadi saa 9.17 alasiri leo ni Mtaturu pekee ndiye alikuwa amerejesha fomu huku wengine 12  wakiwa hawajarejesha.

Wagombea wa vyama vya upinzani 12 waliokwisha kuchukua fomu na wanasubiriwa kurejesha ni; Hamidu Hussein (ADA-Thadea), Tirubya Mwanga (UPDP), Ameni Npondia (CCK), Amina Ramadhan (DP) na Ayuni John (UDP).

Wengine ni Amina Mcheka (AAF), Maulid Mustafa (ADC), Selemani Ntandu (CUF), Feruzy Fenezyson (NRA), Abdallah Tumbo (UMD), Donald Mwanga (TLP) na Masalio Kyara (SAU).

Iwapo  wagombea hao ikifika saa 10 jioni wakiwa hawajazirejesha na mgombea wa CCM Mtaturu ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya Ikungi akawa ametimiza masharti, atatangazwa kupita bila kupigwa kuongoza jimbo hilo lililoachwa wazi na Tundu Lissu.

Lissu ameliacha wazi baada ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kulitangazia Bunge Juni 28, 2019 kwamba mbunge huyo amepoteza sifa kutokana na kutokujaza fomu za mali na madeni ya viongozi wa umma pamoja na kutotoa taarifa kwake (spika) kuwa yuko wapi.

Pia Soma

Lissu amekuwa nje ya Tanzania tangu Septemba 7, 2017 akitibu majeraha ya risasi 16  alizomiminiwa akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria kikao cha Bunge kilichokuwa kikiendelea.

Chanzo: mwananchi.co.tz