Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Meya, diwani waeleza sababu kuondoka CUF, kujiunga CCM

49140 CCM+PIC

Thu, 28 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa meya wa manispaa ya Mikindani wilaya ya Mtwara Mjini, Jofrey Mwanchisye na diwani wa Chikongola wilayani humo, Mussa Namtema wamejiuzulu nyadhifa zao na kueleza sababu za kuachana na CUF na kujiunga na CCM.

Mwanchisye na Namtema walitangaza kujiuzulu nyadhifa hizo jana katika ofisi za CCM wilaya hiyo.

Kujiuzulu kwa Mwanchisye nafasi ya umeya kumekuja siku tano tu tangu aliyekuwa meya wa Ilala (Chadema), Charles Kuyeko kujiuzulu na kujiunga na CCM akisema ameridhishwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli.

Wakizungumza na Mwananchi jana muda mfupi baada ya kutangaza kujiuzulu, Namtema na Mwanchisye walitaja sababu mojawapo ni kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais Magufuli.

“Nimeridhishwa na utendaji wa Rais Magufuli kwani anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi hivyo sioni sababu ya kutomuunga mkono. Nimeona bora nihamie huku, tena nimechelewa kufanya uamuzi huu,” alisema Mwanchisye.

Alisema sababu nyingine ni mwenendo usioridhisha ndani ya CUF, licha ya baadhi ya kesi kuisha na waliokuwa viongozi wa chama akiwamo aliyekuwa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo.

“Kesi zimeisha lakini bado wanaendelea kufuatana fuatana tu na majibizano yasiyo na tija sasa kwa nini niendelee kubaki katika chama hiki. Nimeondoka na kujiunga CCM ambako ni salama na imara,” alisema.

Kwa upande wake, Namtema alisema kwa ufupi: “Nimeridhika na utendaji wa Serikali chini ya Rais Magufuli ndio maana nimeamua kumuunga mkono.”.

Alipotafutwa naibu katibu mkuu wa CUF-Bara, Magdalena Sakaya alisema: “Ni kweli wamejiuzulu lakini sijajua kwa nini wamechukua uamuzi huo.”



Chanzo: mwananchi.co.tz