Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Meya: Nimeondolewa kwa mizengwe, nakubali yaishe

101005 Meya+pic Meya: Nimeondolewa kwa mizengwe, nakubali yaishe

Mon, 6 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe jana alikabidhi ofisi na gari kwa mkurugenzi, Hamid Njovu akisema amekubali kukaa kando ili kupisha shughuli za maendeleo, licha ya kuondolewa kwa mizengwe.

Baada ya kukabidhi ofisi, Kimbe alizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo akiwataka waendelee kuchapa kazi.

Alisema kwamba hawezi kung’ang’ania kupinga kuondolewa umeya licha ya taratibu za kumuondoa kutozingatia kanuni na taratibu, lakini ni lazima akubali ili mambo mengine yaendelee.

“Nimefikiria jambo la muhimu sana nikagundua kwamba Dar es Salaam (baada ya kuondolewa meya) vikao vya madiwani havifanyiki na hivyo maendeleo katika eneo hilo hayatafanyika,” alisema.

“Nilifikiri ningeendelea na ule mgogoro wa kusema niendelee kukaa ofisini, pengine mkurugenzi angeshindwa kuitisha vikao. Lakini pia ambao wangeteseka na kupata shida ni wananchi wa Iringa.

“Itoshe tu kusema jambo lililofanyika juzi mimi nimeridhika nalo na nikaona nipate fursa ya kuzungumza na watumishi niwatie moyo. Mimi ni diwani wa Isakalilo nitaendelea kuwepo katika viwanja vya halmashauri.”

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Alisema jambo kubwa ambalo lilimfanya aongee na watumishi kutaka kuwatoa woga na zile huruma ambazo wanazo kwake na kuwataka wasijisikie vibaya na anawaomba wawe na amani na huru kufanya kazi.

Alisema kwa muda wa miaka minne ya uongozi wake wananchi wanajivunia mazuri ambayo yanaonekana katika Manispaa ya Iringa.

“Kwa miaka mitatu mji wa Iringa umepata hati safi kwa maana ni pamoja na matumizi mazuri ya fedha, tuna miradi mikubwa ya kimaendeleo ambayo Benki ya Dunia imetupatia fedha kwa sababu ya utawala bora na matumizi mazuri ya fedha,” alisema.

Alisema wamejenga shule nyingi za sekondari na msingi na kwa miaka mitatu mfulilulizo katika matokeo ya darasa la saba, Manispaa ya Iringa imekuwa ikishika nafasi ya saba na nane kitaifa.

Akifafanua zaidi kuhusu kuondolewa madarakani bila taratibu kufuatwa, Kimbe alisema: “Ninachokitambua ni nguvu ya polisi, na watawala hawakutamani Manispaa ya Iringa kuwe kuna meya wa Chadema. Kwa sababu hakukuwa na sababu za msingi ambazo zilipaswa ziniondoe. Nilitolewa kwa kura 14 kwa akidi ya kura 26. Ilibidi watu wa kunitoa waanzie 17 kwenda juu.

“Nimekubali yaishe kwa sababu kisheria na taratibu meya hawajamuondoa, lakini kwa mujibu wa nguvu ya polisi na utawala wametaka nitoke.

Alisema kwa kuwa anawapenda wananchi wa Iringa ameamua kukaa kando ili shughuli za maendeleo ziendelee, lakini ataendelea kutoa ushauri kama diwani katika vikao kama ilivyokuwa awali.

Alisema tayari ameshakabidhi gari na ofisi na anachosubiri ni kuendelea na majukumu yake ya udiwani.

Mkurugenzi wa manispaa hiyo alisema tangu Kimbe achaguliwe kuwa meya Desemba 5, 2015 wameshirikiana naye katika mambo mengi.

Alisema akiwa kama kiongozi wao wametengeneza dira ya halmashauri, wametekeleza yale ambayo halmashauri iliyataka.

“Nilihitaji sana hiki kikao (kuongea) na watumishi kwa sababu itatutengenezea daraja,” alisema Njovu.

“Kuna vitu vingi tunavihitaji, wengi tulikuja hapa ni wageni lakini manispaa ilikuwa na uwezo na mipango yao mingi.”

Chanzo: mwananchi.co.tz