Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Meya Jacob atoa vyerehani 10 kwa vikundi vya kina mama

48576 MEYA+PIC

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ameviwezesha vikundi vya kina mama vya manispaa hiyo vyerehani 10 vya kisasa vyenye thamani ya takribani Sh20 milioni ambavyo watavitumia katika shughuli mbalimbali kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Jacob ambaye pia ni diwani wa Ubungo (Chadema), ametoa msaada huo, leo Jumatatu Machi 25, 2019 kwa vikundi viwili vya Mashujaa Women na Victoria Foundation baada ya kukutana na wawakilishi wa vikundi hivyo visivyopungua watu 30 kila kikundi.

Amesema kabla ya kuwakabidhi msaada huo, vikundi hivyo viliandaa maandiko ya mradi wa ushonaji na namna watavyotaka kuwezesha na watakachokifanya baada ya kupata msaada huo.

“Walianza kuja mmoja mmoja ofisini, nikawaambia waunde kikundi ili nijue namna ya kuwawezesha ili wafanikiwe. Huu ni mwanzo na nimezindua tu, fursa ipo wazi kwa wanaotaka vyerehani ambavyo nimevipata kwa ushirikiano na wadau mbalimbali kikiwemo kiwanda cha nguo cha Spesho Tanzania,” amesema Jacob.

Jacob amesema baada ya vikundi hivyo kupata msaada huo wataanzisha kiwanda cha ushonaji nguo kitakachowasaidia kujikwamua kiuchumi kupitia bidhaa watakazokuwa wakizizalisha na kuziuza kwa wadau mbalimbali.

Mkurugenzi wa Mtendaji wa SpeshoTanzania, Jefrey Jesse amesema baada ya kina mama hao kupata msaada huo wao watahakikisha wanawajengea uwezo wa namna ya kuziendesha mashine hizo ili shughuli zao wazifanye kwa ufanisi.

“Hatutawapatia mafunzo ya kushona peke yake, bali pia kuendesha biashara ya ushonaji. Unaweza ukafahamu kushona lakini huwezi kuendesha biashara ya ushonaji, sisi tutawasaidia hili,” amesema.

“Wengi wanajua kuwa natoa mkopo, lakini hili tukio la leo si mkopo bali ni msaada nilioupata nilioutafuta kwa ajili ya kuwasaidia kina mama hawa. Msaada huu wa leo ni sawa na viwanda vidogo viwili vya ushonaji, kazi ambayo itatekelezwa na kina mama hawa mnaowaona hapa,” amesema Jacob.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mwenyekiti wa kikundi cha Victoria Foundation, Bertha Mwakasege alimshukuru Jacob kwa kuwapatia fursa hiyo itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz