Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Meya Dar kusuka, kunyoa leo

91267 Pic+meya Meya Dar kusuka, kunyoa leo

Thu, 9 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkutano maalumu wenye ajenda ya kupokea taarifa ya timu iliyochunguza tuhuma dhidi Meya wa Jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania, Isaya Mwita utafanyika leo Alhamisi Januari 9, 2020 saa 4 asubuhi katika ukumbi wa Karimjee.

Awali kulikuwa na taarifa zinazoeleza huenda mkutano huo maalumu usifanyike badala yake utafanyika kesho Ijumaa kutokana na Mwita kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu kuweza zuio la kutojadiliwa katika kikao chochote kitakachoitishwa.

Hata hivyo, uamuzi huo wa Mahakama unatarajiwa kutolea leo Alhamisi na Hakimu wa Mahakama hiyo, Janeth Mtenga wa kukubali ombi la Meya Mwita au wajibu maombi ambao ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mwita anaomba zuio hilo ili kusubiri hadi kesi ya msingi aliyoifungua mahakamani hapo itakaposikilizwa.

Jana Jumatano wajumbe wa Baraza hilo walipewa taarifa za kutokuwapo kwa kikao hicho kilichokuwa kimeitishwa juzi na Mkurugenzi wa Jiji hilo, Sipora Liana hadi kesho Ijumaa Januari 10, 2020 lakini ilipofika usiku, walipigiwa tena simu wakitaarifiwa uwepo wa kikao hicho.

Akizungumza na Mwananchi, Mwita alisema awali alitaarifiwa kikao kimeahirishwa lakini ghafla usiku wa jana alipigiwa simu kuwa kitafanyika kwa kile alichoelezwa kuwa mahakama haijatoa uamuzi wa zuio lake.

Lengo la kikao hicho cha madiwani ni kupokea taarifa ya uchunguzi dhidi ya tuhuma za Mwita baada ya tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda  kuchunguza tuhuma ambazo zinamkabili.

Miongoni mwa tuhuma anazokabiliana nazo Mwita ni kutotumia Sh5.8 bilioni za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda). Fedha hizo ni asilimia 51 ya hisa zilizotolewa na kampuni ya Simon Group kama sehemu ya ununuzi wa asilimia 51 ya hisa za Uda.

Tuhuma nyingine ni kutumia vibaya gari ya ofisi ambayo alipata nalo ajali, kushindwa kuongoza kikao cha baraza la madiwani na kusababisha meya wa Ubun-go Boniface Jacob kugombana na meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo na kudaiwa kuwapendelea baadhi ya mameya kuingia kwenye kamati za fedha.

Hata hivyo, Mwita ambaye pia mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, alishajibu tuhuma hizo akisisitiza hahusiki na jambo hilo bali ni za kutengenezwa ili kuondolewa katika kiti hicho alichokitumikia kwa miaka minne.

Chanzo: mwananchi.co.tz