Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Meya Dar ajitosa urais CHADEMA

91321 Mwita+pic Meya Dar ajitosa urais CHADEMA

Fri, 10 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

ALIYEKUWA Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, amejitosa katika kinyang’anyiro cha kuomba kuteuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kugombea urais.

Mwita amekuwa mwanachama wa tano kujitokeza kuchukua fomu kutaka kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.

Alichukua fomu hiyo jana ikiwa ni miezi sita baada ya kung’olewa umeya wa jiji hilo Januari 9, mwaka huu, kwa madai mbalimbali ikiwamo tuhuma za matumizi mabaya ya gari la umma kwa kulisababishia kupata ajali.

Tuhuma nyingine zilizomfanya Mwita avuliwe umeya wa jiji hilo ni kushindwa kuongoza kikao cha Baraza la Madiwani na kupendelea baadhi ya mameya kuingia katika kamati za fedha.

Mwita alijitokeza katika ofisi za CHADEMA, jijini Dar es Salaam na kukabidhiwa fomu hiyo na Mkurugenzi wa uchaguzi wa chama hicho, Reginald Munisi.

Baada ya kuchukua fomu hiyo, Mwita aliahidi kuwa endapo chama chake kitampa ridhaa ya kuwania nafasi hiyo, kitu cha kwanza kwenye utawala wake ni kupatikana kwa Katiba Mpya kwa manufaa ya Watanzania wote.

“Katiba Mpya ndilo jambo la kwanza nitakaloanza nalo endapo chama changu kitaniamini na kunipitisha na hatimaye kuwa Rais wa Tanzania. Katiba itaheshimiwa na kila mtu,” alisema Mwita.

Pia alisema atashughulikia tatizo la ajira kwa vijana nchini ambalo linasababishwa na mipango mibaya ndani ya serikali.

Alisema njia atakazotumia kuongeza ajira nchini ni kutumia sekta ya kilimo kuwekeza kilimo cha kisasa kitakachoajiri vijana wengi nchini.

“Endapo chama changu kitanipitisha kugombea urais nitaifanya kazi hii ya kusaidia Watanzania wengi kupata ajira kwa sababu hadi sasa ajira nyingi za wahitimu wa vyuo hazijatoka na Serikali imeshindwa kutumia mbinu za kutatua changamoto hii,” alisema Mwita.

Kadhalika aliahidi kuwa, atatumia uzoefu wake wa kuliongoza Jiji la Dar es Salaam lenye watu zaidi ya milioni saba, kuliunganisha Taifa na kuleta watu pamoja.

“Nyie waandishi ni mashahidi nimekuwa nikitumia burasa kuongoza jiji hili na naamini nitatumia busara hizo kulileta taifa pamoja,” alisema Mwita.

Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu ndiye alikuwa mwanachama wa kwanza kuchukua fomu hiyo Julai 4, kupitia wakala wake David Jumbe. Dk. Mayrose Majinge alikuwa wa pili, alichukua fomu juzi Julai 7, mwaka huu.

Wengine waliochukua fomu hizo juzi ni Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu na Wakili Gasper Mwanalyela.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live