Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Membe kuhojiwa CCM Februari 6

94471 Membe+pic Membe kuhojiwa CCM Februari 6

Wed, 5 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ameitwa kuhojiwa na kamati ya maadili ya CCM.

Mbali na Membe, wengine wanaotakiwa kuhojiwa na kamati hiyo ni makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho tawala nchini Tanzania, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba.

Hata hivyo,  makatibu wakuu hao wa zamani hawajathibitisha kama nao wameitwa kuhojiwa licha ya Desemba 2019 chama hicho kuwataja wote watatu kuwa watahojiwa na kamati hiyo.

Vigogo hao, waliokuwa mjadala hivi karibuni baada ya sauti za baadhi yao kusambaa mitandaoni wakizungumzia kupasuka kwa CCM.

Leo Jumanne Februari 4, 2020 katika wa mtandao wa kijamii wa Twitter uliotumwa na mtu mwenye jina kama la Membe umeeleza kuwa ameitwa kuhojiwa.

“Hatimaye jana jioni nimepokea barua ya kuitwa kwenye kikao cha kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu jijini Dodoma.”

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Kikao kitafanyika Februari 6, 2020  saa 3 asubuhi kwenye jengo la White House. Nitahudhuria bila kukosa na bila kuchelewa! Stay tuned,” amesema Mwanadiplomasia huyo.

Licha ya kutopatikana lakini Membe hutumia akaunti hiyo kueleza masuala mbalimbali, ikiwemo maendeleo ya kesi yake mahakama kuu.

Siku ilipotangazwa kuwa watatu hao watahojiwa, Halmashauri Kuu ya CCM ilieleza kuwasamehe na kuwaonya wabunge wa tatu, January Makamba (Bumbuli), William Ngeleja (Sengerema) na Nape Nnauye (Mtama) ambao kwa nyakati tofauti walimuomba msamaha mwenyekiti wa  CCM, Rais John Magufuli.

Kuitwa kwao kuliibua upya sakata lililoonekana kutulia ndani ya CCM.

Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ali aliwahi kumlaumu Membe kutoonekana tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu. Dk Bashiru, akiwa mkoani Geita, alimtuhumu Membe hadharani kuwa anakwamisha mkakati wa urais 2020 wa Rais Magufuli, huku akimtaka afike ofisini kwake.

Lakini waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje alimjibu kuwa CCM ina utaratibu wake wa kuitana.

Siku hiyo ujumbe  wa Twitter uliotumwa na mtu mwenye jina kama la Membe ulisema atakapokwenda ofisini kwa Dk Bashiru, mtu anay-emtuhumu kuandaa mkakati wa kumng’oa Rais Magufuli, naye awepo ili athibitishe tuhuma hizo.

Hivi karibuni ziliibuka sauti za viongozi mbalimbali, zikiwamo zinazosadikika kuwa ni za wabunge hao, zikizungumzia waraka ulioandikwa na Makamba na Kinana kuhusu uongozi wa CCM kutowalinda dhidi ya vitendo vya kudhalilishwa.

Makatibu hao wa zamani waliandika waraka huo kwa katibu wa Baraza la Ushauri wa Viongozi wa CCM, Pius Msekwa wakizungumzia mmoja wa wanaharakati ambaye amekuwa akiwachafua bila hatua kuchukuliwa.

Makamba na Kinana waliokuwa watendaji wakuu wa chama hicho tawala katika awamu ya nne, walitumia katiba ya CCM, toleo la 2017 ibara ya 122 kuwasilisha malalamiko yao ambayo yalizua mjadala ndani na nje ya chama hicho.

Msekwa aliwaandikia barua vigogo hao akijibu malalamiko yao waliyoyawasilisha kwake wakidai kudhalilishwa kwa mambo ya uzushi, uongo na mtu aliyejitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz