Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Membe achukua fomu za urais NEC

802640b76ba9c41c9a7684ddf06cd8f5 Membe achukua fomu za urais NEC

Sat, 8 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Bernard Membe amechukua fomu kuomba kuteuliwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) ili kuwania kiti cha Urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Membe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa takribani miaka 10 katika serikali ya Awamu ya Nne ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete amechukua fomu akijinadi kwamba hatakuwa rais wa wanyonge pekee bali wa watanzania wote.

Mgombea huyo aliingia Ofisi za NEC Njedengwa jijini hapa jana, akiwa ameambatana na Mgombe Mwenza wake, Profesa Omary Fakih Hamad, Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wengine wa chama na wanachama.

Wengine ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Mhonga Ruhwanya, Katibu wa Mambo ya Nje, Bonifasia Mapunda, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano Janeth Rithe na Katibu wa Ngome ya Vijana Mwanaisha Mndeme na viongozi wengine.

Akitoa maelezo kabla ya kukabidhiwa fomu hizo, Mkurugenzi wa NEC, Dk Wilson Mahera alisema kuwa watatakiwa kudhaminiwa na wapiga kura wasiopungua 200 ambayo wamejiandikisha kupiga kura katika kila mkoa kwenye mikoa 10 na kati ya hiyo, angalau miwili kutoka Zanzibar.

Akikabidhi fomu, Mwenyekiti wa Tume, Jaji (mstaafu) Semistocles Kaijage, alisema pia katika mkoba wa fomu kuna nakala nane za fomu namba 10 ya tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida Mgombea wa Urais, kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU) Mutamwega Magaiwa na mgombea mwenza wake, Safia Berwa na baadhi ya wapambe wa chama hicho walifika katika ofisi za NEC jijini hapa kwa ajili ya kuchukua fomu za kugombea urais huku wakiwa hawajavaa viatu (pekupeku).

Wagombea hao kabla ya kuingia kwenye jengo la Uchaguzi kuchukua fomu wakiwa hawajavaa viatu waliinama na kusujudu ardhi na kisha wakaelekea katika chumba cha kuchukua fomu kilichopo ghorofa ya tatu.

Pamoja na SAU kuchukua fomu jana Agosti 7 vyama vingine vilikuwa vilivyochukua fomu ni ADC na UPDP. Jumatano Agosti 5, mwaka huu ulipoanza mchakato huo, vyama vilivyochukua fomu ni AAFP, DP, NRA. Juzi Agosti 6, mwaka huu ilichukua CCM peke yake.

Chanzo: habarileo.co.tz