Dar es Salaam. Dakika chache baada ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania kumvua uanachama Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, ameibuka na kusema atatoa kauli muda si mrefu.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Membe amesema, “Watanzania wenzangu nimepata habari ya kufukuzwa kwangu kutoka kwenye chama changu cha CCM. Simu zinamiminika hadi nashindwa kuzijibu. Tulieni! Nitapata muda wa kuongea na wote muda si mrefu!”
Wakati Membe akivuliwa uanachama leo Ijumaa Februari 28, 2020, katibu mkuu wa zamani wa chama hicho tawala, Abdulrahman Kinana amepewa karipio na kutakiwa kutogombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho kwa miezi 18 huku katibu mkuu mwingine wa zamani, Yusuf Makamba akisamehewa.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Februari 28, 2020 na katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ndogo za CCM zilizopo mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam.
Polepole alikuwa akieleza uamuzi wa kamati kuu ambayo ilitoa siku saba kwa kamati ya nidhamu iliyowahoji vigogo hao kukamilisha suala lao na kuwasilisha taarifa.
Kinana, Makamba pamoja na Membe walihojiwa kwa nyakati tofauti Dodoma na Dar es Salaam kutokana na kutuhumiwa kwa makosa ya kimaadili.
Habari zinazohusiana na hii
Agizo la viongozi hao kuhojiwa lilitolewa na Halmashauri Kuu ya CCM iliyokutana Mwanza, Desemba 13, 2019. Wakati Membe akihojiwa Dodoma, Kinana na Makamba walikwenda katika ofisi ndogo za Lumumba, mahojiano hayo yaliongozwa na Makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula.
Vigogo hao walihojiwa baada ya sauti zao kusambaa katika mitandao ya kijamii wakieleza jinsi CCM inavyopoteza mvuto na jinsi chama kilivyoshindwa kuwalinda makatibu hao dhidi ya mtu anayejiita mwanaharakati, ambaye alikuwa akitoa tuhuma dhidi yao.
Maamuzi kamati kuu
Polepole amesema kamati kuu imeazimia Membe afukuzwe uanachama, “uamuzi huyu umekuja baada ya kuwa taarifa zake ndani ya chama zinaonyesha mwenendo wake kutoka mwaka 2014 ambako katika chama amewahi kupata adhabu nyingine ambazo zingeweza kumsaidia kujirekebisha lakini imeonekana sivyo.”
“Adhabu ndani ya CCM kuna za siri ambazo ataambiwa mhusika na zinaweza kuwa za wazi. Adhabu ya karipio na kufukuzwa zinasomwa hadharani.”
Amesema kamati kuu imepokea maelezo ya Kinana na imeazimia apewe adhabu ya karipio kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za chama hicho toleo la 2017.
“Adhabu ya karipio imeanishwa katika kanuni na inasema, ‘mwanachama anayefanya kosa linalokipata matope chama na bila kuonyesha nia ya kujirekebisha basi kamati kuu inaweza kumpa mwanachama huyo adhabu ya karipio’.”
“’mwanachama aliyepewa adhabu ya karipio atakuwa katika hali ya matazamio kwa muda usiopungua miezi 18 kutoka tarehe ya leo (Februari 28, 2020) ili kumsaidia mwanachama huyu katika jitihada za kujirekebisha. Akiwa katika kipindi hicho hatakuwa na haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika chama lakini atakuwa na haki ya kupiga kura kuchagua viongozi wa chama kama ana dhamana hiyo.”
Kuhusu Makamba amesema, “baada ya fuatilia, kumhoji na kufuatilia mwenendo wake, kamati kuu imeazimia kwa kauli moja kwamba Makamba asamehewe makosa yake aliyotenda.”
“Imetoa msamaha huu kwa misingi kuwa Makamba wakati wote tangu aliposomewa mashtaka yake amekuwa mtu muungwana, mnyenyekevu na mtii kwa mamlaka ya chama. Kubwa kuliko yote ameomba msamehewe makosa yake kwa barua zilizoambatanishwa katika maelezo yake. Amesamehewa makosa yake.”