Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mdude asimulia waliomteka, asema hatabadili msimamo

58734 Pic+mdude

Tue, 21 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwanaharakati wa Chadema, Mdude Nyagali amesema kutekwa kwake na watu wasiojulikana hakutamrudisha nyuma na kumfanya abadili mwenendo wake wa kukosoa kuhusu masuala mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mdude alisema hakuna kitu atakachobadilika kwa kuwa haoni kosa lake na ataendelea kukosoa hata kama ataonekana anatumika.

“Mimi siwezi kubadili msimamo wangu, mimi ndio nimezaliwa hivi. Kifo huwa kinatisha sana lakini ni kizuri ukiwa unawapigania wanyonge na watu ambao hawawezi kusema, kifo ni kibaya kama unakufa unawadhulumu wanyonge,” alisema.

Alisema anashangazwa na upotoshaji unaofanyika kwamba tukio la kutekwa kwake halihusiani na siasa wakati watekaji walikuwa wakimshambulia kuhusu itikadi za kisiasa.

“Hawa wanaosema kwamba tukio langu si la kisiasa kwanini wang’ang’anie nyaraka za chama, mahakama na laptop yenye vitu vyangu binafsi. Kwanini waniambie EU, Mbowe na Lissu waje wanisaidie kwa madai kwamba tunatumiwa na mabeberu.”

Mdude alikwenda mbele zaidi na kueleza kuwa hana mpango wa kuhama nchi kwa kuhofia kupotezwa kwa sababu ya tukio hilo.

Habari zinazohusiana na hii

“Ninachojua nilitekwa kwa sababu ya itikadi za kisiasa ila kwa kuwa mimi ni Mtanzania siwezi kuhama nchi kwa sababu ya hofu nitaendelea kuvumili mpaka mwisho kama Yesu,” alisema Mdude bila ya kutaja wanasiasa gani au chama gani kimehusika na kutekwa kwake.

Kufuatia tukio hilo Mdude ametaka uchunguzi wa tukio hilo la kutekwa kwake ufanywe na vyombo huru vya uchunguzi ili kuwabaini waliomteka.

Chanzo: mwananchi.co.tz