Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mdee na wenzake wakaribishwa ACT-Wazalendo

MDEE NA WENZAKEEE Mdee na wenzake wakaribishwa ACT-Wazalendo

Fri, 29 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha ACT-Wazalendo, kimefungua milango kwa wabunge viti maalum 19 waliofukuzwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wajiunge nacho.

Wito huo umetolewa leo tarehe 29 Disemba 2023 na Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo,Ado akizungumza na Mwanahalisi Online ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo amesema kuwa, chama chao kipo tayari kuwapokea hususan kiongozi wao Halima Mdee, kwa kuwa ni majembe.

Ado Shaibu “Tukimuona mtu ni jembe mathalani kina Halima Mdee wana mgogoro na chama chao wakiamua kwamba wanataka kujiunga na ACT-Wazalendo, tutawapokea na kuwapa nafasi sababu tunaamini wanasifa,” amesema Ado.

Ado amesema “katika siasa wanasiasa wanaweza kujikwaa kwa hili na lile, chama kinabidi kipime na nikitazama wanawake hawa 19 ni ishara ya ukomavu.”

Ado ametoa wito huo wakati akizungumzia athari za kupokea wanasiasa kutoka vyama vingine, ambapo amesema kitendo hicho kiliwaathiri baada ya kumpokea aliyekuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Hayati Benard Membe, kisha kumteua kuwa mgombea wake urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, ambapo baadae alirejea alikotoka.

“Tumejifunza juu ya hilo, kitendo cha Membe kurejea CCM kinapaswa kutufundisha vyama vya upinzani kwamba ni lazima kwa nafasi nyeti ya urais tuandae makada wetu watakaokuwa tayari kuvumilia changamoto za upinzani badala ya kila baada ya uchaguzi wanarejea CCM,” amesema Ado.

Hata hivyo, Ado amesema ACT-Wazalendo iko tayari kupokea wanachama kutoka vyama vingine kisha kuteua kuwa wagombea baada ya kuwafanyia tathimini ya kina kuona kama wanafaa, lakini hakiko tayari kupokea mwanachama wa chama kingine kisha kuwateua kuwa wagombea urais wa chama hicho.

Hatua ya ACT-Wazalendo kuwafungulia milango wabunge hao viti maalum waliofukuzwa Chadema Novemba 2020, imekuja wiki mbili baada ya Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, kutoa hukumu dhidi ya kesi waliyofungua kupinga kuvuliwa uanachama.

Mahakama hiyo iliamuru Chadema kuitisha tena kikao cha Baraza Kuu lake kwa ajili ya kusikiliza tena rufaa zao za kupinga kufukuzwa ili haki itendeke.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live