Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mdee ana kesi kujibu tuhuma uchochezi

Halimamdee Mdee ana kesi kujibu tuhuma uchochezi

Fri, 29 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imesema Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, anayekabiliwa na kesi ya uchochezi ana kesi ya kujibu dhidi ya tuhuma hizo.

Kadhalika, imesema itaanza kusikiliza ushahidi wa utetezi Juni 25 na 26 na mshtakiwa anatarajia kuita mashahidi watano.

Uamuzi huo, ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wao.

Awali, upande wa Jamhuri ulidai kuwa kesi hiyo imepangwa kwa ajili ya kusikiliza uamuzi wa kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la.

Hakimu Simba alisema, mshtakiwa ana kesi ya kujibu hivyo mahakama yake itaanza kusikiliza ushahidi wa utetezi Juni 25 na 26, mwaka huu.

Mashahidi watatu wa upande wa Jamhuri wametoa ushahidi akiwamo Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Urafiki, Mrakibu wa Polisi (SP), Batseba Kasanga.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Julai 3, 2017 katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), iliyopo Mtaa wa Ufipa, Wilaya ya Kinondoni, Mdee anadaiwa kutamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa: ‘Anaongea ovyo ovyo, anatakiwa afungwe breki’ kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Mdee alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka yake Julai 10, 2017 na yupo nje kwa dhamana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live