Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mdee aitega Chadema

Mdee.png Halima Mdee

Sun, 17 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati mjadala ukiendelea wa uamuzi wa Mahakama Kuu kufuta uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema, dhidi ya waliokuwa wanachama wake 19 wa kuwafukuza uanachama, Halima Mdee ameonesha matumaini yake juu ya kumalizika kwa mgogoro huo. Mdee aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema

(Bawacha), amesema wanachama wengi wa Chadema, wanatamani mgogoro huo umalizike lakini kuna wachache kwa maslahi yao hawatamani kuona hilo likitokea.

Mbunge huyo wa viti maalum alisema hayo jana jijini hapa, ikiwa ni siku takribani tatu tangu Mahakama hiyo kutoa uamuzi huo wa kutengua uamuzi wa Baraza Kuu na kuibua mjadala wa kipi kinaendelea baada ya hapo.

Mjadala huo unatokana na uamuzi wa Mahakama kuielekeza Chadema kwenda kupitia upya rufaa hizo, huku ikisisitiza umuhimu wa haki asili iwepo kwa wajumbe wa Kamati Kuu walioshiriki kuwafukuza Mdee na wenzake 18 kwamba wasiwe sehemu ya Baraza Kuu.

Kamati Kuu ya Chadema Novemba 27, 2020 iliwafukuza Mdee na wenzake wakituhumiwa kujipeleka bungeni kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum, wakati chama hicho kikidai hakikuwa kimewateua kwenye kikao chochote kwenda kuwa wabunge.

Alichosema Mdee Mwananchi ilizungumza na Mdee kujua nini kinaendeleaje baada ya uamuzi huo wa Mahakama, ambapo alisema kwa sasa hawezi kuzungumza lolote kuhusu kinachofuata kwa kuwa bado hawajakaa na kujadiliana na mawakili wao.

Hata hivyo, kama yeye binafsi, alisisitiza kuwa ana imani mwisho wa mgogoro huo utaisha na watarudi pamoja, kwani kuna watu wengi wanaotamani uishe isipokuwa wachache kwa maslahi yao.

Mdee alisema mgogoro huo hautaisha kwa kuzungumza zungumza kwenye vyombo vya habari na kwamba kwa watu wazima tofauti zinatatuliwa kwa kukaa ndani kujadiliana na kufikia maafikiano.

"Kwa hiyo mimi naamini huko mbele tutafika vizuri na kama kuna watu ambao wanatamani huu mgogoro usiishe watakuja kushangaa tu wao wenyewe, kwa sababu wengi wanatamani uishe lakini kuna wachache wenye maslahi yao hawatamani uishe," alisema Mdee na kuongeza:

"Kwa ufupi kuna wachache hawatamani mambo yaishe lakini kuna wanacChadema wengi tu wanatamani mambo yaishe ili tuweze kusonga mbele kama timu, wengi sana. Kwa hiyo mimi naamini hatimaye wengi watawazidi wachache ndio maana mimi huwa sipendi kuzungumzazungumza ovyo."

 

Mtazamo wa Chadema

Kutokana na maelezo hayo ya Mdee, gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na mambo ya Nje, John Mrema kupata mtazamo wa chama hicho kuhusu hoja ya kulimaliza suala hilo.

Alisema: “Kipimo cha kuwapima hao wana-Chadema wengi na wachache unakitoa wapi, sijajua kama wamehojiwa. Lakini wao wanapaswa kujua chama kilikwishawafukuza tangu Novemba 27 mwaka 2020.

Alisema baada ya kufukuzwa walikwenda mahakamani na Mahakama imejiridhisha Kamati Kuu ilifuata utaratibu wa Katiba na sheria za nchi, hivyo alisema wanachopaswa kujua wao si wabunge halali.

Katika kusisitiza hilo, Mrema alisema: “Hawana chama wanachokiwakilisha kwa hiyo wapo huko kwa maslahi yao binafsi.

Wanajua wanachokifanya hakiko halali na wanabebwa tu.Kwa hiyo wao ndio waamue sisi kama chama tulikwisha kuamua na kuwafukuza na Mahakama imethibitisha walifukuzwa kihalali. Wasianze kusingizia wana-Chadema wengi na wachache.’’

Juzi Wakili kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Fulgence Massawe, aliunga mkono uamuzi wa Mahakama kuwa si vema wajumbe wanaofanya uamuzi kwa masuala ya nidhamu au hadhi ya uanachama wakashiriki pia kufanya uamuzi katika ngazi ya rufaa kwa uamuzi unapopingwa.

Hivyo alisema huo ni ujumbe kwa Msajili wa Vyama vya Siasa anaposajili aangalie na Katiba zao kuona kama zina namna nzuri ya kutatua migogoro.

Massawe alisema LHRC imekuwa ikipendekeza kuwe na Baraza Huru la Usuluhishi wa Migogoro ndani ya Vyama vya Siasa na si walewale wanaaoshtaki ndio wanageuka kuwa majaji kama ilivyokuwa Kwa kina Mdee.

Akizungumzia maoni hayo ya Wakili Massawe, Mdee aliunga mkono akisema alichokisema Massawe na la Mahakama ilivyolielezea suala hilo ni jambo lenye mantiki.

"Ina mantiki sana kwamba katika mfumo wa utoaji haki, common sense ni hiyo kwa sababu unapokaa katika vikao kama mahakama ni tofauti na unapokaa kwenye vikao vingine vya kujadili masuala ya kawaida," alisama

Alisema ni kwa sababu hiyo kwenye haya mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa majadiliano yanaendelea nadhani hilo ni miongoni mwa vifungu ambavyo vinaangaliwa.

Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu (CC), Esther Matiko na Ester Bulaya; aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.

Wengine, ni aliyekuwa Katibu mkuu wa Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA), Nusrat Hanje; aliyekuwa Naibu katibu mkuu wa Bawacha (Bara), Jesca David Kishoa; Cecilia Pareso, Agnesta Lambart, ambaye alikuwa mwenezi wa Bawacha na Tunza Malapa, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, mkoani Mtwara.

Katika orodha hiyo, wamo pia Asia Mohammed, aliyekuwa Naibu Katibu mkuu wa Bawacha (Zanzibar), Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live