Dar es Salaam. Wabunge watatu wa Chadema wameshindwa kutolewa leo Jumatano Machi 11, 2020 katika gereza la Segerea kwa kile kinachoelezwa kuwa mkuu wa gereza hilo kuwa na kikao.
Wabunge hao ni Halima Mdee (Kawe), Ester Matiko (Tarime Mjini) na Ester Bulaya (Bunda).
Wabunge hao na wenzao watano akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walipelekwa gerezani jana kutokana na kushindwa kulipa faini ya Sh320 milioni, baada mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kuwatia hatiani na kuwahukumu katika mashtaka ya uchochezi yaliyokuwa wakiwakabili.
Wakili wa washtakiwa hao, Fred Khiwela ameiambia Mwananchi leo, Machi 11, 2020, saa 11:30 jioni kuwa tayari wameshakamilisha taratibu zote ikiwemo kulipa faini ya jumla ya Sh110 milioni kwa wabunge hao.
Khiwelo amesema kutokana na wateja wake kushindwa kutolewa leo, wamejipanga kesho asubuhi kuwatoa.
Mwananchi iliweka kambi karibu lango la kuingilia gerezani na kubaini kuwa licha ya mkuu wa gereza kuwa na kikao, washtakiwa hao wameshindwa kutolewa kunatokana na wao kuchelewa kufika gerezani, hali iliyopeleka muda wa kazi kuisha.
Habari zinazohusiana na hii
- VIDEO: Mashinji atoka jela baada ya CCM kumlipia faini ya Sh30 milioni
- VIDEO: CCM wakamilisha kumlipia Mashinji faini ya Sh30 milioni
- Chadema waanza mchakato kuwatoa gerezani Halima Mdee, Matiko na Bulaya
- Zitto awachangia Chadema Sh2 milioni
Kwa upande wake, Matiko alitiwa hatiani katika mashtaka matatu, hivyo kutakiwa kulipa faini ya Sh 30 milioni
Washtakiwa hao na wenzao walitiwa hatiani katika kesi ya uchochezi.