Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge wa Ukerewe atinga bungeni, iliibua suala la MV Nyerere

27213 Mkundi+pic TanzaniaWeb

Thu, 15 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mbunge wa Ukerewe (CCM), Joseph Mkundi ameingia kwa mara ya kwanza bungeni leo na kuibua suala la kupinduka kwa kivuko cha MV Nyerere.

MV Nyerere ilipinduka Septemba 20 katika ziwa Victoria kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoa wa Mwanza na kusababisha vifo vya watu 230 na manusura 41 na wakati huo Mkundi alikuwa Mbunge kupitia Chadema.

Oktoba 11 Mkundi alitangaza kujiuzulu na kuondoka Chadema kisha kuhamia CCM ambako alipitishwa kugombea tena katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 2. Hata hivyo, Mkundi amepita bila kupingwa na leo  ameapishwa na Spika Job Ndugai.

Katika kipindi cha maswali, Spika Ndugai alimpa fursa ya kuuliza swali ambapo Mbunge huyo aliitaka Serikali kutoa majibu ya lini itapeleka gari la wagonjwa katika kisiwa hicho kwani ilipozama MV Nyerere wananchi walipata shida kwa kukosa gari la wagonjwa katika kituo cha afya cha Bwisya.

Akijibu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliahidi kupeleka gari la wagonjwa katika kipindi kifupi kwani Serikali inajiandaa kununua magari ya wagonjwa 70.

Mbunge mwingine mpya wa Serengeti (CCM), Ryoba Chacha ambaye naye alijiuzulu ubunge akiwa Chadema na kutimukia CCM na leo kuapishwa, aliuliza kama Serikali itakubali kuwajengea barabara ya lami kilomita nne katika mji wa Mugumu.

Akijibu, Naibu Waziri wa Tamisemi, Josephati Kandege alisema Serikali kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) itafanya kazi hiyo kwa kuwa wananchi wameonyesha uungwana kwa kumchagua Mbunge huyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz