Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Ruth Mollel ameshauri Serikali ya Tanzania kuweka nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa Serikali kwa sababu wana hali mbaya.
Ruth ametoa kauli hiyo leo Jumanne Februari 4, 2020 wakati akichangia taarifa tatu za utekelezaji wa shughuli za kamati za Utawala na Serikali za Mitaa, Katiba na Sheria pamoja na Sheria Ndogo.
Katibu mkuu huyo wa zamani wa utumishi amesema ni wakati muafaka kuweka bajeti ya nyongeza ya mshahara kwa watumishi kwa sababu hali zao ni mbaya.
Ruth amesema katika taarifa zote alizosoma hakuna sehemu wamezungumzia kundi kubwa la watumishi wa umma ambalo ni raslimali watu.
Amesema kwa muda wa miaka minne hawajawahi kuongezewa mishahara na kwamba hilo jambo amekuwa akilisema mara nyingi.
“Ni wakati muafaka sasa Serikali katika bajeti ijayo kuweka mishahara kwa ajili ya kuwaongezea watumishi ambao hali zao ni mbaya na wanahitaji kuboresha maisha yao,” amesema.
Pia Soma
- Utata kifo cha Mwalimu kinavyowapasua kichwa Jeshi la Polisi
- Hakimu ataka kesi ya Mo Dewji kuendelea bila washtakiwa wengine
- Dk Bashiru aonya kauli tata za makada CCM
Ametoa mfano wa Askofu wa Kanisa Katoliki Ngara, Severin Niwemugizi kwamba hawezi kutoka nje ya nchi kwa sababu amenyang’anywa hati yake ya kusafiria.
Kauli za mbunge huyo zilimnyanyua Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama ambaye alitoa taarifa kwa mbunge huyo akifafanua kuwa taratibu za utendaji kazi wa Baraza la Mawaziri zimefuatwa, kila jambo linalohusu utendaji limewekewa utaratibu.